Kesi ya Aveva: Meneja wa Barclays aeleza Aveva alivyofungua akaunti na kuhamisha fedha

Muktasari:

Mbali na Aveva vigogo wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni aliyekuwa Makamu wa wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Dar es Salaam. Meneja wa benki ya Barclays tawi la mikocheni Prisca Daudi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba,  Evans Aveva ni mteja wa benki hiyo.

Prisca alidai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati akitoa ushahidi.

Akiongozwa na Wakili kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Leonard Swai, Prisca alidai Aveva ni mteja wake ambapo alifungua akaunti katika tawi la Mikocheni.

Alidai katika taratibu zakufungua akaunti mteja anatakiwa kupeleka picha yake ili kujua kama yeye ndio muhusika, kitambulisho pamoja na barua kutoka serikali ya mtaa au kwa mwajiri wake.

Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa Novemba 20, 2014 Aveva alifungua akaunti iliyokuwa na nyaraka kutoka klabu ya Simba ikionyesha kipato chake kwa mwezi ni Sh 8 milioni.

Prisca alidai Machi 16, 2016 ziliingia pesa kwenye akaunti ya mteja wake ambaye ni Aveva kiasi cha dola 300,000 kutoka benki ya CRDB.

Aliendelea kudai fedha zinapozidi kiasi zinapoingia kwenye akaunti ni lazima kukaa na kujiridhisha pesa hizo ni za nini.

Prisca ambaye ni shahidi wa tatu alidai fedha hizo zilionyesha ni malipo ya mkopo yaliyokuwa yanalipwa na klabu ya Simba kutoka benki ya CRDB kwenda kwenye akaunti ya Aveva.

Alidai kuwa Aprili 4, 2016 fedha kiasi cha dola elfu 62 ziliamishwa kutoka kwenye akaunti ya Aveva na kulipwa kwenye kampuni ya China kwaajili ya kulipia nyasi.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 10, mwaka huu kwaajili ya kuendelea nakuutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi ili imalizike kwa wakati.

Mbali na Aveva vigogo wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni aliyekuwa Makamu wa wake, Geofrey Nyange maarufu (Kaburu) na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 ikiwemo kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi,  kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.

Katika shtaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, inadaiwa Machi 15, 2016 katika benki ya Barclays Mikocheni, Dar es Salaam alijipatia Dola za Kimarekani 187,817, takriban Sh 400 Milioni kutoka katika Timu ya Simba wakati akijua zimetokana na zao la kosa la kughushi.

Katika shtaka la kughushi linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh 90 Milioni huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika shtaka lingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya March10 na September 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.