MAONI: Taifa Stars ni wazi imeshikilia furaha, huzuni ya Watanzania

Tanzania leo ipo katika maombi na subira ya tukio moja la timu yao ya Taifa, Taifa Stars itakapokuwa na dakika 90 nzito za kuibeba nchi na kuipa furaha ama machungu.

Ni baada ya miaka 39, leo Taifa Stars inarudi uwanjani kuanzia saa 12:00 jioni kusaka pointi tatu zitakazowarudisha tena katika ramani ya kushiriki Fainali za Mataifa Afrika mwaka huu nchini Misri.

Historia inaonyesha mara ya mwisho Stars kushiriki fainali hizi ilikuwa ni mwaka 1980 na wachezaji wa kikosi hicho wote sasa ni rika la mababu wakibaki kama washauri kwa vijana wacheza soka.

Baada ya hapo, haikuwahi kutokea nafasi nyingine kwa Stars kuvuzu ikiwa nji sawa na umri wa mtu mzima mwenye familia na hata mjukuu mmoja. Miaka 39 sio midogo.

Ni kipindi kirefu Watanzania wamekuwa wakikosa nafasi hii na kuishia kujitafutia timu za kushangilia kila michuano hii inapofika. Wengi wamekuwa wakiyashangilia mataifa ya Kaskazini na Magharibi ambayo yako juu kisoka.

Ilibidi utumwa kama huo uitawale nchi yetu na hadi sasa ikiwa ni miaka 39 na Watanzania wakichukulia ni kawaida kutokana na taifa lao kushindwa kushiriki michuano hiyo huku pia wakiona hakuna ndoto kama hiyo.

Hata hivyo, nafasi pekee ya kufuta taswira hiyo ni leo pale kwenye Uwanja wa Taifa, Taifa Stars itakapomenyana na Uganda ambao tayari wameshajikatia tiketi ya kushiriki mashindano hayo makubwa Afrika, zitakazofanyika nchini Misri Juni mwaka huu. Matumaini ya Watanzania yapo kwa kikosi cha Taifa Stars wakiongozwa na nahodha wao Mbwana Samatta ambaye kwa kauli yake amethibitisha ‘Wanajeshi wenzake wako tayari kwa vita’.

Mechi ya leo imekuwa ikiwapa hamasa wananchi kwa takribani wiki nzima. Hii ni kutokana na uzalendo waliokuwa nao na juu ya umuhiumu wa mechi hiyo ambayo kwa hakika itaweka historia mpya nchini.

Ni dhahiri uwanja utafurika watazamaji kwa ajili ya kuishangilia timu yao na huo ndiyo uzalendo wa kweli kutokana na hata waliopanga viingilio walikuwa wazalendo, baada ya kuweka viingilio vya chini, pia watu na kampuni mbalimbali wamekuwa wakinunua tiketi nyingi na kuzigawa bure.

Wakati huo huo, huko kwenye kambi ya Stars maandalizi yamekuwa yakifanyika kwa akili ya mbali chini ya Kocha Emmanuel Amunike kuhakikisha ushindi unapatikana.

Stars inatakiwa ipate ushindi na hicho ndicho Watanzania wanasubiri, pia wakisubiri kujua matokeo ya mchezo wa Cape Verde dhidi ya Lesotho ambao nao kila mmoja ana nafasi yake katika kufuzu.

Kama Stars itashinda leo kisha Cape Verde na Lesotho wakapata sare basi nafasi itakuwa ni kwa Tanzania kurejea kwenye ramani ya fainali hizi. Stars inachotakiwa kutambua ni Watanzania wanawaombea wao kuhakikisha wanashinda na juhudi na utulivu wao wa akili basi utaweza kulifanya Taifa kulipuka kwa furaha wakisheherekea mafanikio ya nchi yao.

Wachezaji Stars wanatakiwa kutanguliza masilahi ya Taifa kwa kushirikiana uwanjani kuanzia kuokoa, kutengeneza nafasi na hata kufunga kwani kama itapata mabao mengi, itasaidia kurahisisha kupata ushindi.

Zawadi pekee ambayo wachezaji wa Stars wanaweza kuwapa Watanzania na kubaki katika mioyo yao ni kupatikana kwa ushindi kwenye mechi hii.

Wachezaji wanatakiwa kutoweka akili yao kuwa mechi inaweza kuwa nyepesi kutokana na Uganda kufuzu bali wachukulie mchezo huu kwa Uganda ni kama nao wanataka nafasi.

Uganda wanataka kulinda heshima yao, pia wachezaji watataka kutafuta nafasi ya kuwepo katika kikosi chao kitakachokwenda Misri. Hatutakiwi kudharau, Stars ikapambane kiume kutafuta ushindi kwa namna yoyote ndani ya uwanja na uwezo huo wanao ndiyo maana Watanzania watakuja kwa wingi.

Hii itakuwa heshima kwao kama wachezaji na makocha kutokana na kuwa kikosi cha pili kuipeleka Tanzania katika fainali za mwaka huu. Itakuwa ni simanzi kubwa kwa Stars kushindwa mchezo wa leo, pia kukosa tiketi ya kufuzu huu utakuwa ni msiba mkubwa kwa taifa kwa jinsi watu walivyohamasika. Hakuna kitakachoibeba Stars leo zaidi ya kila mchezaji atakayepata nafasi kujitolea mpaka nafasi yake ya mwisho kulitetea taifa lake.

Watanzania twendeni Taifa tukawape nguvu wachezaji wetu lakini pia Stars tambueni tunakuja hebu tupeni raha Watanzania kukata tiketi ya kwenda Misri,tunaamini mnaweza mtafanikiwa, Insha Allah.