Kiungo Serengeti anogewa na Mo Banka

KATIKA soka kila mchezaji anakuwa na mchezaji wake, ambaye anamvutia na muda mwingine hufikia hatua ya kumuiga kila ambalo anafanya.

Jambo hilo limetokea kwa kiungo wa Serengeti Boys, Charles Masenga ambaye alikiri wazi kuwa anavutiwa na kiungo wa Yanga, Mohammed Issa ‘Banka’.

“Banka kiukweli napenda jinsi anavyokuwepo uwanjani kuanzia uchezaji wake mpaka anavyojipanga, na kuna vitu ambavyo najifunza nikimuangalia anapokuwa uwanjani,” alisema.

Masenga aliongeza kwa upande wa viungo wanaocheza nje ya Tanzania anavutiwa na Paul Pogba anayecheza timu ya Taifa Ufaransa na Manchester Utd.

“Pogba anajua kukaba lakini pia anajua kushambulia, uchezaji wake unanivutia na huwa namuangalia namna ambavyo anacheza kwa sababu mimi mwenyewe ni kiungo. Natambua kuwa jitihada zangu ndio zinaweza kuniwezesha kufikia mafanikio yao uwanjani,” alisema.