Namungo yatanguliza mguu mmoja Ligi Kuu

Muktasari:

Namungo ndio timu pekee kwenye Ligi Daraja la Kwanza ambayo haijapoteza mechi yoyote msimu huu ikiwa imecheza michezo 17

Dar es Salaam. Bao la dakika ya 58 lililofungwa na Luca Kikoti limeiweka Namungo FC katika mazingira mazuri ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao kupitia kundi A baada ya kufikisha pointi 47.

Goli hilo lililotokana na mkwaju wa penalti, liliiwezesha Namungo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Reha FC kwenye Uwanja wa Chuo cha Bandari Temeke.

Matokeo hayo yameifanya Namungo iongeze pengo la pointi baina yake na Mbeya Kwanza inayoshika nafasi ya pili hadi kufikia pointi nane.

Timu hiyo sasa inahitajika kuibuka na ushindi kwenye mechi tatu kati ya tano ilizobakiza ili ipande Ligi Kuu msimu ujao.

Kocha msaidizi wa Namungo FC, Bakari Malima 'Jembe Ulaya' alisema baada ya ushindi huo akili yao wanaelekeza kwenye mechi ijayo.

"Tunamshukuru Mungu tumepata ushindi japo mechi ilikuwa ngumu. Changamoto kubwa leo ilikuwa ni wachezaji kutokuwa makini kwani tungeibuka na ushindi mkubwa lakini hata hayo matokeo tuliyoyapata yanatosha.

Kwa sasa tunakwenda kujipanga kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Dar City ugenini huko Tanga," alisema Jembe Ulaya