Saa mbili zatumika kuamua uchaguzi Yanga

Muktasari:

Yanga ilitakiwa kufanya uchaguzi wao wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi Januari 13, lakini uliahirishwa baada ya baadhi ya wanachama kupeleka kesi mahakamani kupinga mchakato wa uchaguzi.

Dar es Salaam. Vuguvugu la uchaguzi wa Yanga linafikia tamati kesho baada ya kamati ya uchaguzi kukaa kikao cha takribani saa mbili kuanzia saa 9:15 alasiri hadi 11:16 jioni kuamua namna ya kufanya uchaguzi upya.

Awali uchaguzi ulisimamishwa baada ya baadhi ya wanachama kwenda kupinga kufanyika uchaguzi huo, lakini kamati imeamua kutangaza siku ambayo itatumika kwaajili ya uchaguzi.

Kikao hiko kilichukua takribani saa mbili baada ya kukubaliana baadhi ya vitu, ndipo walipokubaliana na kutoka nje ya kikao hiko kwa furaha na amani.

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa TFF, Ally Mchungahela aliliambia Mwanaspoti, baada ya kukaa kikao na wajumbe wa Yanga wamepanga tarehe ya uchaguzi wataitangaza kesho Machi 6.

"Tumekaa na wenzetu na tumekubaliana kwamba kesho tutatangaza siku ambayo uchaguzi utafanyika kama kawaida, hakuna tatizo lolote lile," alisema.

Kikao hiko kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi klabu ya Yanga, Venance Mwamoto, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Siza Lyimo na Mjumbe wa kamati ya uchaguzi wa Yanga, Seif Gulamali.