MTIHANI: Hukumu ya Sarri, Solskjaer ipo darajani

Muktasari:

Endapo Chelsea itatupwa nje katika michuano ya FA huku ikitupwa nje ya Top Four mwishoni mwa msimu kuna uwezekano mkubwa Sarri akafukuzwa hata kama ataiwezesha Chelsea kuchukua kombe la Ligi

London, England. Kuipa uzito mechi ya keshokutwa Jumatatu kati ya Chelsea na Manchester United katika pambano la FA, wabashiri wa mambo wanaamini pambano hilo huenda likatoa hukumu kwa makocha wa pande zote mbili katika hatima zao na klabu zao.

Chelsea itaikaribisha Manchester United katika dimba la nyumbani Stamford Bridge baada ya kuitupa nje Sheffield Wednesday katika pambano la mwisho huku United ikiichapa Arsenal katika uwanja wake wa nyumbani wa Emirates.

Kwa upande wa Chelsea kocha, Maurizio Sarri amekalia kuti kavu baada ya Chelsea kupepesuka katika msimamo wa Ligi mpaka nafasi ya sita baada ya kupokea kipigo cha aibu cha mabao 6-0 kutoka kwa Manchester City Jumapili iliyopita.

Kipigo hicho ni kikubwa cha kwanza kwa Chelsea kwa kipindi cha miaka 28 na kimemuacha Sarri akiwa hoi na analitegemea zaidi pambano la kesho katika kurekebisha mambo kabla panga la tajiri wa timu hiyo, Roman Abramovich halijamuangukia.

Endapo Chelsea itatupwa nje katika michuano ya FA huku ikitupwa nje ya Top Four mwishoni mwa msimu kuna uwezekano mkubwa Sarri akafukuzwa hata kama ataiwezesha Chelsea kuchukua kombe la Ligi ambapo imefika na watacheza na Manchester City mwishoni mwa mwezi huu.

Chelsea bado ipo katika michuano ya Kombe la Europa lakini mpaka sasa bado safari ni ndefu kufikia kilele cha michuano hiyo na Sarri anaweza kufukuzwa hata Mei kama Chelsea itadorora zaidi katika Ligi pamoja na kutupwa nje na United katika pambano la kesho.

Kwa upande wa United, kocha Ole Gunnar Solskjaer naye ana mtihani mgumu wa kuendelea kuwashawishi matajiri wa kazi wampe kibarua hicho moja kwa moja baada ya kutwaa kiti kutoka kwa kocha, Jose Mourinho desemba mwaka huu.

Solskjaer ameanza kuonja machungu ya kukalia kiti cha Old Trafford baada ya Jumanne usiku United kuchapwa mabao 2-0 nyumbani Old Trafford na PSG katika pambano la kwanza la mtoano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Pambano hilo lilichukuliwa kama kipimo kikubwa kwa Solskjaer kuelekea kupewa kiti hicho jumla lakini ilidhihirika bado ana kazi ngumu ya kufanya kukisuka kikosi cha United kuelekea katika mafanikio baada ya makocha watatu waliopita, David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho kuchemsha.

Kocha huyo Mnorway ambaye ni staa wa zamani wa United ana kazi ngumu ya kubadilisha matokeo ya pambano hilo mnamo Machi 6 mwaka huu lakini kwanza atalazimika kufanya kazi ngumu ya kuitupa Chelsea kesho kwa ajili ya kurudisha Imani ya matajiri wake.

Endapo Solskjaer atatupwa nje ya michuano ya FA Imani ya mashabiki na matajiri dhidi yake itaanza kupungua kutokana na United kujikuta katika mazingira ya kutolewa katika michuano miwili ndani ya siku tano.

Katika Ligi Kuu ya England, Solskjaer kwa kiasi kikubwa amepambana kuirudisha United Top Four lakini mpaka sasa mchuano ni mkali baina yao na Arsenal na Chelsea ambazo nazo zinapambana kuitaka nafasi hiyo adimu.

Wakati Arsenal na Chelsea zikiweka walau tumaini la kuipata nafasi hiyo kupitia michuano ya Uefa, United inalazimika kuichukua nafasi hiyo moja kwa moja kwa sababu matumaini ya kuchukua taji la Ulaya yanaelekea kufa.

Haya yote yanatokea wakati Solskjaer akiwa katika vita kubwa ya kuiwania nafasi ya ukocha wa kudumu na kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino ambaye naye anapigiwa upatu kuichukua nafasi hiyo huku akionekana kukubalika na wengi ndani ya Old Trafford.