Kwa rekodi hii: Yanga, Simba nani kucheka Uwanja Taifa

Monday February 11 2019

 

Dar es Salaam.Huko mtaani unaambiwa licha ya mashabiki kulijadili na kutaniana kuhusu mechi ya kesho ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba dhidi ya Waarabu, Al Ahly ya Misri, lakini ukweli akili zote na hata mioyo inadunda kuelekea pambano la Watani wa Jadi litakalochezwa Jumamosi hii.

Simba na Yanga zitavaana kwenye Uwanja wa Taifa, katika pambano lao la 102 tangu kuasisiwa kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965.

Tayari ile presha ya pambano hilo imeanza mapema, huku kila upande ukijitutumua ukitamba kuwa lazima chama lao liibuke na ushindi Jumamosi.

Kwa mujibu wa rekodi zilizopo ni kwamba katika mechi 101 za timu hiyo likiwamo la mwisho lililopigwa Septemba 30, mwaka jana na kumalizika kwa suluhu, Yanga bado ni wababe dhidi ya Simba kutokana na kushinda mara 36. Simba imeitambuia Yanga mara 30 tu, huku mechi 35 zikimalizika bila kutoa mshindi.

Mbali na kuongoza kwa kushinda mechi nyingi, lakini Yanga pia imewaburuza watani wao kwa kufunga mabao mengi katika mechi hizo, kwani imetupia kambani mara 107, huku nyavu zao zikitikiswa mara 96 na Mnyama.

Katika mechi hizo 101, Yanga imekusanya alama 143 dhidi ya 125, licha ya kwamba kwa miaka ya nyuma timu inayoshinda ilikuwa ikinyakua pointi mbili kabla ya kubadilishwa na kuwa alama tatu kwa kila mchezo ambayo timu inashinda.

Je, Simba watashuka uwanjani Jumamosi ili kuwanufaisha Yanga ama itapunguza deni la vipigo na mabao kwa Vijana wa Jangwani? Tusubiri!

Msimamo mechi za watani tangu 1965-2018

               P       W    D     L      F      A     PTS

YANGA 101   36   35   30   107 96   143

SIMBA  101   30   35   36   96   107 125

Advertisement