Samatta azidi kushangaza, Ndemla akiduwaza wengi

Muktasari:

Samatta aliandika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano hiyo ya pili mikubwa kwa klabu barani Ulaya.

Dar es Salaam.Wazungu wamepagawa. Wazungu wagumu Halafu sasa ni kwamba hawakuanza kupagawa jana au juzi. Walianza kupagawa naye kitambo. Ndio maana haikushangaza sana, kuamua kumuimba wakati akiwapa raha uwanjani.

 Simzungumzii Mohamed Salah wa Liverpool aliyeimbwa na mashabiki wa klabu yake msimu uliopita wakati akiiongoza timu yake kuwaadhibu Man City kwenye Uwanja wa Anfield katika mechi ya Ligi Kuu ya England iliyoisha kwa watetezi hao wa EPL kulala 4-3.

Hapa namzungumzia kijana kutoka Mbagala, kule TMK kunakochukuliwa poa na baadhi ya watu. Mbwana Samatta amezidi kuwatia uchizi mashabiki wa soka wa Genk, pale Ubelgiji. Amezidi kuwashangaza wazungu kwa namna anavyotupia mabao kambani.

Wazungu na kiburi chao chote walishindwa kujizuia kwa straika huyo Mtanzania. Bila kulazimishwa na mtu waliamua wenyewe kumuimbia wimbo. Samagol...Samagol...Sama...Samagol lalaaaaa...! Ni sauti za mashabiki wazungu waliokuwa wakimuimba Samatta, usiku wa Agosti 31 mwaka jana baada ya kutupia kambani hat trick wakati wakiivusha Genk kutinga makundi ya Ligi ya Ulaya (UEFA Europe Legue) msimu uliopita. Samatta alikuwa akiiadhibu Brondby IF ya Denmark. Ni nadra sana kutokea.

Samatta aliandika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano hiyo ya pili mikubwa kwa klabu barani Ulaya.

Lakini kama ulidhani, wimbo ule na sifa nyingine alizokuwa akipewa zilimfanya abweteke, pole yako. Samatta anazidi kuwapagawisha Wazungu.

Usiku wa juzi, aliifunga mabao mawili wakati timu yake ya Genk ikiizamisha Standard Liege kwa mabao 2-0. Genk ilikuwa Uwanja wa nyumbani wa Luminus, mjini Genk.

Moja alifunga dakika ya 67 akimalizia mpira wa krosi ya nahodha wake Alejandro Pozuelo iliyopanguliwa vibaya na kipa Guillermo Ochoa kutoka Mexico.

Dakika tatu kabla ya kumalizika kwa pambano hilo alitupia jingine akiitendea vyema pasi ndefu ya Joakim Maehle na kufumua shuti lililomshinda kipa wa Liege. Hilo lilikuwa bao lake la 19 msimu huu katika Ligi Kuu ya Ubelgiji (Jupiler League).

Kama hujui ni straika mmoja tu Ulaya aliyemfunika Samatta (kabla ya mechi za jana Jumamosi). Ni Lionel Messi tu wa pale Barcelona.

Mchawi huyo wa kutupia nyavuni kutoka Argentina ana mabao 21. Mawili zaidi na aliyonayo Samatta. Yaani nyota wengine wote unaokinukisha Ulaya wanaisoma namba kwa mtoto wa Mbagala.

Si Mo Salah, wala Romelu Lukaku ama Neymar, wote wamefunika (hii ni kabla ya mechi za jana). Ni kweli Ligi ya Ubelgiji haifanani na zile tano maarufu za Ulaya, lakini bado Samatta amaewakimbiza.

Wanasubiri kwa Samatta aliyeiwezesha Genk kukaa kileleni kwa muda mrefu kwa tofauti nyingi dhidi ya wapinzani wao.

Kwanini Samatta asishangaze? Hakuna Mtanzania aliyewahi kucheza Ligi ya UEFA wala kuwa kinara wa mabao, lakini Samatta kaweza.

Kama Samagol angekuwa amewahi kucheza Ulaya kabla ungesema uzoefu unambeba. Lakini ni kwamba alipotimkia TP Mazembe akitokea Simba mwaka 2011 na kukipiga kwa misimu mitano alionwa na Genk.

Huu ni msimu wake wa nne akiwa ameichezea klabu hiyo jumla ya mechi 109 za Ligi Kuu na kuifungia mabao 45. Rekodi zinaonyesha Nahodha huyo wa Tanzania ameichezea Genk jumla ya mechi 146 za mashindano yote na kuifungia mabao 61.

Itachukua muda rekodi yake kuja kuvunjwa na wachezaji wa Kitanzania. Hakuna anayeonekana ana mzuka wa kufikia alipo Samatta.

Watanzania wana kila sababu ya kujivunia kwa kile anachokifanya Samatta. Straika huyo ameiwakilisha vyema nchi na kuipeperusha bendera ya Tanzania.

Haitashangaza kuona msimu ujao, Samatta akiuzwa klabu kubwa Ulaya. Wazungu wamepagawa naye kwanini wasimgombee?! Dirisha lililopita ilikuwa kidogo tu atue England kukinukisha EPL kupitia Cardiff City. Wacha Wazungu wamuimbe. Anastahili!

Lakini wakati Samatta akizidi kuwashangaza Wazungu, kuna nyota mwingine mkali ameduwaza Watanzania. Huyu ni Said Ndemla.

Ni bonge la kiungo aliyeibuliwa na kulelewa Msimbazi. Ndemla anajua mpira bwana. Ana nguvu za kupiga mashuti tofauti na mwili wake. Ndio maana haikushangaza Yanga kwenye dirisha la usajili mwanzoni mwa msimu walikuwa wakimnyatia ili wambebe, kabla ya Simba kuamua kumbakisha kikosini.

Kwa wanaokumbuka mwaka juzi alienda kufanya majaribio ya klabu ya AFC Eskilstuna ya nchini Sweden. Tulifahamishwa alifuzu majaribio yake.

Hata hivyo hakuondoka kwenda kuichezea timu hiyo hadi mwezi uliopita aliitwa tena nchini humo.

Akili za wengi walidhani alikuwa akienda kujiunga jumla kuichezea timu hiyo. Lakini ni kwamba klabu ile ile ya AFC ilimtaka aende kufanya tena majaribio na ikadokezwa kila kitu poa na kilichobaki ni mazungumzo tu ili aachiwe akakipige kule. Ghafla juzi kati kaibuka tena Boko Veterani kwenye mazoezi ya Simba.

Kitu gani kilichomkumba mchezaji huyo? Hakuna mwenye jibu, kwa vile si yeye wala mabosi wake wa Msimbazi walio tayari kueleza kilichomkumba kijana huyo.

Ngoja tuone nini kitakachoendelea, ila ukweli kwa soka na kipaji alichojaliwa Ndemla, kwa sasa angekuwa kule walipo kina Farid Mussa ama Yahya Zayd.

Kijana anajua soka, sema tu hana bahati hata ndani ya kikosi cha Msimbazi, kwani mara nyingine anaanzia benchi. Kwanini? Msiniulize, tuendelee kuduwaa kwa pamoja!