Kagere aja na mapya Simba

Muktasari:

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ameibuka na mtindo mpya wa kushangilia lengo likiwa ni kuwapagawisha mashabiki wake

Dar es Salaam. STRAIKA wa Simba, Meddie Kagere alianza na staili yake ya ushangiliaji ya kuziba jicho moja na kudai kwamba staili hiyo anamaanisha umoja na mshikamano kwa wachezaji wote ila sasa amekuja na staili mpya ya kufunika macho yote kwa mikono miwili.

Staili hiyo aliifanya wakati timu yake ikicheza na Mbabane Swallows ya Eswatin katika mechi yao ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Simba ilishinda bao 4-1.

Kagere ameeleza kwamba staili hiyo inamaanisha kwamba hata bila kuona ana uwezo wa kumfunga kipa yoyote; "Nilikuwa na maana kwamba hata bila kuona huyo kipa ningemfunga tu."

Kagere ambaye ni baba wa watoto wanne ambao mmoja ni wa kiume aitwaye Nasri Kagere (6), watatu wa kike ambao ni Keza Tiana (4) na mapacha Ariana na Aribah Kagere wenye mwaka mmoja na miezi mitano.

Straika huyo raia wa Rwanda hadi sasa ameifungia Simba mabao saba sawa na Emmanuel Okwi pamoja na Said Dilunga wote wa Simba na Harriet Makambo wa Yanga.

Imeelezwa kwamba ana staili nyingi za ushangiliaji, hivyo mashabiki wa soka nchini hasa Simba watapata burudani nyingi kutoka kwake.

Straika huyo kwasasa anasakwa na timu mbili Vita Club ya DR Congo na Zamaleki ya Misri na yupo tayari kuondoka endapo tu watafikia makubaliano kati ya Simba na timu hizo kwani ana mkataba wa zaidi ya mwaka mmoja.

Kagere alisaini mkataba wa miaka miwili ameanza kutumikia msimu huu wenye thamani ya zaidi ya Sh 100 milioni na mshahara Sh 13 milioni kwa mwezi.