Zitto ajitosa sakata la Manji Yanga atoa neno

Muktasari:

Yanga inajianda kufanya uchaguzi wake Mkuu Januria 13, huku kukiwa na malumbano juu ya nafasi ya mwenyekiti igombewe au iachwa kwa Manji

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini na shabiki wa Simba, Zitto Kabwe ameiangalia Yanga inavyolumbana kwenye mchakato wa Uchaguzi wa kuziba nafasi za uongozi klabuni kwao na kuwapa ujanja Wana Jangwani.

Zitto alisema ili Yanga iendelea kubaki kuwa timu kubwa na yenye ushindani, lazima ikubali kuingia kwenye mfumo wa kisasa utakaoifanya klabu yao kuendeshwa bila kumtegemea mfuko wa mtu mmoja.

Mwanamichezo huyo alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa nini mtazamo wake juu ya kinachoendelea Yanga na anadhani Wanayanga wafanye nini ili kuendelea kutisha kama moja ya klabu kubwa na kongwe nchini.

Zitto alisema lazima Yanga ikubali kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu yao hata kama sio lazima wafuate mfumo wa Hisa ulioingia Simba hivi karibuni chini ya bilionea Mohammed 'Mo' Dewji.

"Klabu ya Yanga ni klabu kubwa na inaweza kuleta ushindani kwenye soka iwapo itaongozwa vizuri. Ningependa Yanga iendelee kuwa klabu ya Wananchi lakini iendeshwe kisasa. Sio lazima wawe kama Simba ya sasa, Lakini wanaweza kuendeshwa na menejimenti ya kukodisha (management contract)

Kabla ya jibu hilo, Zitto alitania kama Yanga wanashindwa kuendesha mambo yao ni vyema tu wakaiuza klabu yao kwa watani wao, Simba ili mambo yaende.

"Unawashauri nini, ili waweze kuingia katika mchakato wa mabadilioko kama ilivyokuwa kwa watani zao Simba?" Ndilo swali aliloulizwa na yeye kujibu kwa kifupi; "Waiuzie Simba timu."

Yanga imekuwa kwenye mgogoro na Shirikisho la Sokla Tanzania (TFF) wakipinga uamuzi wa kumkataa kumtambua Mwenyekiti wao, Yusuf Manji aliyekuwa amejiuzulu Mei 20 mwaka jana kabla ya wanachama kumgomea.

Wanachama walimgomea kujiuzulu kwake na hivi karibuni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Kapteni George Mkuchika alitangaza kurejea kwa Manji ikiwa ni siku chache tangu TFF itangaze uchaguzi wa klabu hiyo ukihusisha nafasi ya Uenyekiti, Makamu wake na nafasi nne za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.

UChaguzi huo wa Yanga umepangwa kufanyika Januari 13, mwakani na leo ndio ilikuwa mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu na imeelezwa wagombea zaidi ya 30 wamejitokeza wakiwamo 25 wa kamati ya Utendaji na wanne katika nafasi za Uenyekiti na wengine wanne pia wanaogombea umakamu mwenyekiti.