Mtanzania afanya maajabu Olimpiki Argentina

Muktasari:

Muogeleaji Sonia Tumiotto ameweka rekodi katika michezo ya Madola ya vijana inayoendelea nchini Argentina. Sonia, alimaliza wa kwanza katika mtindo wa freestyle mita 100, baada ya kuongoza kundi lake kwenye mchujo Jumatatu wiki hii.

 

Dar es Salaam. Licha ya kukosa nafasi ya kufuzu kucheza nusu fainali, muogeleaji wa Tanzania, Sonia Tumiotto ameweka rekodi kwa Afrika katika michezo ya Olimpiki ya vijana inayoendelea nchini Argentina.

Sonia amekuwa Mwafrika pekee aliyemaliza wa kwanza katika mtindo wa freestyle mita 100, baada ya kuongoza katika kundi lake kwenye mchujo (heat), juzi Jumatatu.

Katika mashindano yaliyofanyika bwawa la kuogelea la Parque Polideportivo Roca katika mji wa Buenos Aires, Sonia aliyetumia saa 1:01:47 aliachwa kwa sekunde sita na muogeleaji aliyetumia muda bora katika hatua ya makundi kwenye mtindo huo.

Kocha wa timu ya Tanzania Michael Livingstone alisema pamoja na Sonia kutopata nafasi ya kutinga nusu fainali, ameboresha muda wake.

"Katika kundi lake amekuwa wa kwanza, huo ni mwanzo mzuri ingawa ushindani ulikuwa mkali kwenye makundi mengine na walichoangalia siyo nafasi ni muda aliotumia kuogelea ambao kulinganisha na waogeleaji wa makundi mengine haukumuwezesha kufuzu nusu fainali," alisema Livinstone.

Juzi usiku muogeleaji mwingine wa Tanzania, Denis Mhini alikuwa akichuana kwenye mtindo wa freestyle mita 100 akisaka nafasi ya kufuzu nusu fainali.

Waogeleaji hao watachuan katika mtindo wa backstroke kati ya kesho na keshokutwa kusaka tiketi ya kucheza nusu fainali kwenye mashindano hayo yanayoshirikisha waogeleaji 390 kutoka mataifa 139.

Mbali na waogeleaji, wanariadha wa Tanzania, Regina Mpigachai na Francis Damiano wataanza kusaka medali kesho kwenye Uwanja wa Parque Polideportivo Roca.

Wanariadha 680 wanatarajiwa kuchuana kusaka medali za michezo hiyo huku Tanzania ikichuana katika mbio za mita 800 na 3000.