Bocco: Wawa ni mtu wa kazi

Muktasari:

  • Mshambuliaji John Bocco aliyecheza na Wawa wakiwa Azam FC, alimzungumzia jinsi beki huyo anavyojua kukaba na kuokoa hatari mbele ya washambuliaji makini kwa kujiamini na kwamba atakuwa msaada mkubwa katika safu ya ulinzi.

Dar es Salaam. Ujio wa aliyekuwa beki wa Azam FC, Pascal Wawa ndani ya kikosi cha Simba, umetafsiriwa kama ukombozi kutokana na namna ambavyo amewahi kuonyesha kiwango cha juu katika Ligi Kuu Bara, kabla ya kutimkia El Mereikh ya Sudan.

Mshambuliaji John Bocco aliyecheza na Wawa wakiwa Azam FC, alimzungumzia jinsi beki huyo anavyojua kukaba na kuokoa hatari mbele ya washambuliaji makini kwa kujiamini na kwamba atakuwa msaada mkubwa katika safu ya ulinzi.

"Ninavyomfahamu Wawa ni mtu makini katika kazi zake, anajua kuwajibika ipasavyo anapokuwa kwenye mazoezi ya timu na yake binafsi, naamini kuja kwake Simba kuna kitu kitaongezeka katika safu ya ulinzi.

"Pia, ni mchezaji anayependa kucheza kwa kiwango cha juu na mshauri kwa chipukizi kuwaelekeza kuwa na mtazamo wa kucheza soka la kisasa pindi wanapokuwa wanapewa nafasi, hivyo bila shaka atakuwa mfano wa kutosha kwa wengine,"anasema Bocco.

Pia, amewashauri chipukizi wanaocheza nafasi ya Wawa, kutulia na kujifunza uzoefu wake, akiamini utawasaidia kufika mbali zaidi.