Benchikha ndo basi tena Simba, aaga wachezaji

Muktasari:

  • Benchikha alitambulishwa Simba, Novemba 28 mwaka jana akichukua nafasi ya Roberto Oliveira 'Robertinho' aliyefutwa kazi baada ya timu hiyo kufungwa 5-1 na Yanga katika Kariakoo Dabi ya Novemba 5.

Kocha Mkuu wa Simba,  Abdelhak Benchikha inadaiwa amemalizana na klabu hiyo baada ya kuipa Kombe la Muungano na Bodi ya Wakurugenzi imekubali uamuzi wa kocha huyo kutaka kuondoka.

Benchikha alitambulishwa Simba, Novemba 28 mwaka jana akichukua nafasi ya Roberto Oliveira 'Robertinho' aliyefutwa kazi baada ya timu hiyo kufungwa 5-1 na Yanga katika Kariakoo Dabi ya Novemba 5.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa, kocha huyo kabla ya mchezo wa fainali Kombe la Muungano aliongea na wachezaji kuwa huo ndio mchezo wake wa mwisho wafanye kila linalowezekana waweze kumpa heshima.

“Kocha tayari ameshaagana na wachezaji na amewashukuru kwa kumpa heshima kwa kutwaa taji la Muungano chini yake, huku akiwapongeza kwa kufanya kile alikuwa anatamani wakifanye,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kocha amesema alikuwa na muda mzuri ndani ya Simba na anashukuru anaondoka na heshima ya taji baada ya wachezaji wake kupambana na kufanya kwa usahihi maelekezo yake na hatimaye kutwaa taji amewatakia kila la kheri kwenye mapambano ya mechi za ligi zilizobaki.”

Katika mchezo wa fainali Kombe la Muungano, ambao Simba iliifunga Azam kwa bao 1-0 viongozi wa Msimbazi walioudhuria ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) Imani Kajula.

Mbali na kubeba taji, Simba ilitwaa tuzo zote za michuano ikiwamo Mchezaji Bora iliyoenda kwa Fabrice Ngoma, Kipa Bora iliyobebwa na Ayoub Lakred na Nyota wa Mchezo huo alikuwa ni Saido Ntivazonkiza.

Kocha huyo aliyeachana na USM Alger ya kwao Algeria baada ya kuipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na Super Cup alitua Dar es Salaam usiku wa kuamkia Novemba 28.