Yanga waanza na winga wa Zahera

MASHABIKI wa Yanga tayari wameshajua orodha ya mastaa wa kigeni ambao msimu ujao watakinukisha Jangwani, lakini sasa wanatakiwa wakae mkao wa kula kutokana na mabosi wa klabu hiyo kuhamishia nguvu zao kwa wazawa na tayari wameanza na winga wa Mwinyi Zahera.

Kocha huyo wa zamani aliwahi kutokwa povu baada ya kushindwa kumnasa winga, Charles Ilamfya aliyekuwa Mwadui na kunaswa kiulaini na KMC, kumbe mabosi wa Yanga bado wanakumbuka namna Mkongo huyo alivyowaka na sasa wameanza kumfuatilia winga huyo.

Mwanaspoti imedokezwa kwamba Yanga wamemfuata mchezaji huyo na kuanza naye mazungumzo ili kuhakikisha safari hii anatua Jangwani baada ya msimu uliopita kupigwa chenga na kuhamia KMC kutoka Mwadui alikoonwa na Zahera aliyetupiwa virago Yanga Novemba mwaka jana.

Yanga inamtaka winga huyo ili aweze kufanya kazi na Mkongomani Tuisila Kisinda ambaye mipango inaelezwa imekaa poa, lakini pia imepania kuboresha kikosi chao kwa wachezaji bora wazawa na Ilamfya ni mmoja wao ambaye amekubalika na mabosi wa klabu hiyo.

“Tumeshaanza kuzungumza naye ni kama tumerudi upya tu kuna makosa yalifanywa na wenzetu huko nyuma, kazi yetu ni kusahihisha tu ili aje kwetu msimu ujao,” alisema bosi huyo aliye katika Kamati ya Usajili ya klabu hiyo.

“Ni winga mzuri ana kasi na akili akiwa uwanjani tunahitaji kuwa na wachezaji bora katika kikosi chetu ngoja kwanza tupambane naye kuweza kumchukua.”

Ilamfya anayetajwa pia kunyatiwa na Simba alimfanya Zahera kuwa mbogo kwa mabosi wake akiwalalamikia hadharani kwa uzembe waliofanya ikiwamo kumdanganya mpaka mchezaji huyo kuchukuliwa na KMC wakati walikuwa wakimweleza kila kitu kipo sawa kwa winga huyo.

Kwenye mechi za timu yake wiki iliyopita, Ilamfya alionyesha kiwango cha hali juu dhidi ya Yanga wakati Jangwani wakilala 3-0 akifunga moja na kutengeneza jingine na pia kuwatungua Simba wakati KMC ikilala 4-2 kwenye mechi zao za kirafiki kujiandaa na Ligi Kuu Bara.

“Juzi tulikuwa tunamuangalia tena kwa umakini sana wakati anatufunga kuna watu tunaowaamini walimkubali uwezo wake wakisema ni mchezaji mzuri sana.”

MSIKIE KOCHA

Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amesema mikononi mwake mpaka sasa ana orodha ya majina 10 ya wachezaji anaotaka kuwaongeza kikosini kwa msimu ujao, lakini mipango yake ni kusajili sita tu.

Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa huenda wakatua Jangwani ni Michael Surpong kutoka Rayon Sport ya Rwanda, Mpiana Mozizi (DC Motema), Tuisila Kisinda ambao ni wa kigeni na orodha ya wazawa imekuwa ikihusishwa na Ilamfya, Reliants Lusajo na beki wa kushoto wa Polisi Tanzania, Yassin Mustafa ‘Evra’ anayetajwa pia kuwindwa na Azam FC.

“Katika ya wachezaji hao sita watakaosajiliwa Yanga kwa msimu ujao watakuwa kwenye kiwango cha kina Bernard Morrison, Papy Tshishimbi na Lamine Moro kwa ajili ya kuisaidia timu kwa mechi za ndani na zile za kimataifa,” alisema Eymael, kocha raia kutoka Ubelgiji.