Yanga waache ujanja ujanja katika haya

Thursday May 21 2020

 

By Edo Kumwembe

YANGA imeachwa pointi 20 na watani wao Simba. Inashangaza. Ni pointi nyingi. Hata hivyo kwa walioitazama Yanga jinsi ilivyooendeshwa msimu huu ni wazi kwamba kuna mambo wanahitaji kuyafanya kwa ajili ya kupunguza pengo lao na watani wao msimu ujao. Ni mambo ya ndani na nje ya uwanja. Hayahepukiki.

Waende katika mabadiliko ya kweli

Hili haliepukiki kwa sasa. Natabiri mikwamo ya hapa na pale mbele ya safari. Mabadiliko halisi katika mpira wa kisasa ni pamoja kuipeleka timu katika mikono ya watu wachache. Ni wazi kwamba ule msemo wa ‘Timu ya Wananchi, wamiliki ni wananchi’ inabidi uende kwa njia tofauti. Klabu inapaswa kumilikiwa zaidi na watu wachache wenye nguvu ya kipesa ambao wataiendesha kifaida zaidi. Wajaribu kuangalia kina Real Madrid wanachofanya licha ya kile kinachoitwa kwamba ni timu inayomilikiwa na wanachama. Florentino Perez na watu wachache ndio kila kitu.

Hawatafika bila ya kikosi cha kina Kamusoko

Simba wajanja. Walipoona wanataka kwenda katika mabadiliko walihakikisha wanakuwa na timu nzuri ya kuwalainisha mashabiki. Kama unafungwa ovyo mashabiki hawawezi kuamini sana katika mabadiliko yenu unayotaka kufanya. Inabidi ulazimishe ubingwa. Inabidi ulazimishe utemi. Ndani na nje ya uwanja. Meddie Kagere akifanya kazi yake vema uwanjani, basi keshokutwa katika mkutano wa mabadiliko viongozi wanapata nafasi nzuri ya kuongea wanachotaka kuongea. Msimu ujao utakapoanza Yanga watakuwa bado wapo mwanzo mwanzo wa mchakato wa mabadiliko. Wanahitaji kuwa na timu ya kuwalainisha wanachama wawe na raha wakati wakipitisha mabadiliko. Wanahitaji timu kama ile ambayo ilikaribia kumtoa Al Ahly kwake miaka michache iliyopita. Ilikuwa na mafundi wengi. Kina Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Juma Abdul, Amis Tambwe, Kevin Yondani, Simon Msuva na wengineo. Wengine bado wapo lakini hawapo katika ubora ule.

Wamchukue Bakari Mwamnyeto

Advertisement

Na hapa katika kutengeneza kikosi chao wanahitaji kuijenga bila ya ubahili. Nasikia wanabishana na Coastal Union kuhusu mlinzi anayeitwa Bakary Nondo Mwamnyeto ambaye ameanza kujihakikishia nafasi katika timu ya taifa. Ni mlinzi ambaye pia amekuwa akitajwa kwa wapinzani wao Simba. Baada ya kumtazama Mwamnyeto katika mechi za Taifa Stars nadhani hizi kelele zinamstahili. Sina uhakika na dau lake lakini nina uhakika na kiwango chake. Wamchukue. Anaweza kutengeneza ukuta mzuri kwa kuanzia pale Jangwani kando ya Lamine Moro. Baada ya hapo waangalie maeneo mengine. Yanga wasiogope kununua wachezaji wazuri kama kina Kevin Kijiri kutoka KMC. Na wawe makini kuchukua wachezaji kutoka nje. Walete watu wa aina ya Ben Morrison.

Wasake mrithi halisi wa Tambwe

Heritier Makambo alijitahidi kufunga mabao mengi katika msimu wake wa mwisho akiwa na Yanga kabla ya kuondoka na kutimkia klabu ya Horoya huko Afrika Magharibi. Lakini kabla yake kulikuwa na mtu anaitwa Amis Tambwe katika ubora wake. Aliwahi kutishia rekodi ya Mohamed Hussein Mmachinga aliyefunga mabao 26 ndani ya msimu mmoja hapo zamani. Tambwe alifunga mabao 21 ya Ligi msimu wa mwaka 2015/16. Yanga wanahitaji mshambuliaji wa aina hii msimu ujao. Wasijidanganye kwa David Molinga. Timu kubwa hazina muda wa kumsubiri mchezaji. Vipi kwa Ditram Nchimbi? Ni mchezaji mzuri lakini Yanga wanahitaji mshambuliaji mwingine mwenye uhakika wa kuwapa mabao zaidi ya 20 ya msimu. Mshambualiji ambaye atakuwa alama zaidi kisha akacheza sambamba na kina Nchimbi.

Kigamboni isiwe maneno matupu

Yanga wamepewa eneo kubwa kule Kigamboni na Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda. Huwa najiuliza, ule mradi wa ujenzi wa viwanja pale Yanga unaweza kuanza kabla ya mwekezaji mpya wa Yanga kupatikana kupitia mabadiliko? Swali gumu. Hawa viongozi wa sasa watatudanganya tu. Mishahara ya wachezaji iliwashinda. Nadhani waanze na mabadiliko halafu wakishaelewana kuhusu mabadiliko, na nani apewe timu, basi atakayepewa timu awaongoze katika kujenga ‘Yanga Kigamboni Complex’. Wakati wa utawala wa Yusuph Manji nadhani alikuwa anafanya makusudi kujaribu kulazimisha kujenga Uwanja wa Kaunda. Alikuwa anapoteza muda kwa makusudi. Timu yenye hadhi ya Yanga inahitaji viwanja vya mazoezi kama vitatu, bwa-wa la kuogelea, chu-mba vya mazoezi ya viungo, eneo la mchanga wa mazoezi, na mambo mengi. Unayapataje pale katika jengo lao?

Yanga inanusa nusa tu mitandaoni

Upepo wa uwanjani huwa unasambaa kwa mashabiki, halafu unasambaa mitandaoni. Kipindi cha miaka mitatu ambacho Simba imekuwa juu ndani ya uwanja kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kujijenga mitandaoni. Yanga bado wapo nyuma. Kwa mfano, katika mtandao maarufu wa Instagram Simba wana wafuasi, 1.3 milioni. Yanga ina wafuasi 582,000. Kwanini pengo ni kubwa? Mashabiki wa Yanga hawamiliki simu za kisasa? Hapana. Mashabiki hawaoni haja ya kuifuatilia sana timu yao kwa sababu haifanyi vizuri. Yanga inafungwaje 3-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa halafu mashabiki wakataka kufuatilia habari zao mitandaoni? Masuala haya ya juu niliyoandika katika kuimarisha Yanga yanaweza kusabisha Yanga iwe imara na kuwafanya mashabiki wake watiririke mitandaoni kuifuatilia.

Advertisement