Yanga: Chongeni tu, tukutane FA

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael amesisitiza kwamba wanaelewa hali waliyonayo mashabiki wao kutokana na kelele zinazopo mitandaoni, lakini akasema watafanya kitu kwenye Kombe la FA.

Amesema akili yao kwa sasa licha ya kwamba, wanataka kumaliza ligi kwa heshima lakini hesabu ziko kwenye kulipa kisasi dhidi ya Kagera Sugar na kutinga nusu fainali ya Kombe la FA.

Yanga itacheza na Kagera Sugar Jumanne ijayo katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) na mshindi wa mchezo huo atakutana nusu fainali na mshindi wa mchezo kati ya Simba na Azam.

Eymael amewataka mashabiki wa klabu hiyo kutulia na kuendelea kuiunga mkono kwani wao sio Barcelona, Real Madrid wala Liverpool ambayo ina uhakika wa kupata matokeo kila siku katika ligi zao.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji, alisema hakuna mechi rahisi kwao kwani wapinzani wanapambana utafikiri wanacheza na Liverpool kumbe ni Yanga tu.

“Bado tunaendelea kupambana kwani kila mechi ni ngumu kwa sababu hatuna Lionel Messi, Cristiano Ronaldo au Mo Salah kwani ukiwa na watu kama hao basi unaweza kutegemea lolote.

“Wapinzani wetu wamekuwa wakitukamia sana na mara zote wanapambana kama wanacheza na Liverpool kumbe sisi ni Yanga tu,” alisema Eymael.

“Tunaendelea na mapambano bila kukata tamaa, mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono na sisi tutaendelea kupambana ili kuwapa burudani.”

Kocha huyo alisema licha ya kwamba wameukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini wanataka kumaliza nafasi ya pili na ikishindikana basi ya tatu.

“Tunaangalia zaidi Kombe la Shirikisho. Tuna mechi dhidi ya Kagera Sugar moja ya timu bora na ngumu kwenye ligi kwani, wiki iliyopita waliifunga Azam FC na hata sisi waliwahi kutufunga kwa mabao 3-0 hivyo, mechi itakuwa ngumu kwelikweli.

“Ni mechi ya kulipiza kisasi kwani lazima tushinde ili tusonge mbele katika mashindano hayo kwa sababu tunahitaji kuwa mabingwa ili kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa,” alisema Eymael ambaye amepanga kusajili wachezaji watano wapya wa kigeni huku akipukutisha wazawa wasiopungua tisa kwenye kikosi chake.

Amewahi kukaririwa akisema kwamba, msimu ujao anataka kuuanza kwa staili tofauti kabisa.