Xavi awasubirisha stendi Barcelona

BARCELONA, HISPANIA. GWIJI wa Barcelona, Xavi amegoma kurudi kuinoa timu hiyo kwa sasa akiwaambia mabosi wasubiri hadi mwisho wa msimu.

Miamba hiyo ya Nou Camp ilimpa ofa ya mkataba wa miaka miwili na nusu kiungo huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 39 ili akajiunge na timu yao baad ya kocha wa sasa Ernesto Valverde kuwa kwenye presha kubwa.

Barca wapo tayari kumfuta kazi Valverde na walimfuata gwiji wao ili kuwasaidia kurudi kwenye ubora wao kutokana na mambo kwenda hovyo siku za karibuni.

Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Eric Abidal na Ofisa Mtendaji Mkuu, Oscar Grau walikwenda kukutana na Xavi huko Doha baada ya kuchapwa 3-2 na Atletico Madrid kwenye Spanish Super Cup huko Saudi Arabia, Alhamisi iliyopita.

Mazungumzo hayo yaliripotiwa kumshawishi Xavi kukubali kwenda kufanya kazi huko Nou Camp, lakini kwa mujibu wa radio RAC 1 ya Hispania imesema kwamba staa huyo amewaambia mabosi wa timu hiyo wasubiri hadi msimu umalizike.

Hata hivyo, hakutoa maelezo mengi sana, akisema baada ya timu yake anayoinoa kwa sasa Al Sadd kuichapa Al Rayyan.

“Siwezi kucheza kitu, tulifanya mazungumzo na kujadili vingi. Samahani siwezi kuwaambia zaidi. Siwezi kuficha ndoto zangu za kwenda kuwa kocha wa Barcelona. Nimesema hili mara nyingi nna kila mtu anafahamu kwamba naishabiki Barcelona kutoka moyoni kabisa,” alisema Xavi. “Lakini kwa sasa nafanya kazi hapa, nafanya kwa ubora wangu, nilituliza akili yangu kwa ajili ya nusu fainali na sasa tumeingia fainali.”

Thierry Henry, Ronald Koeman na Roberto Martinez wametajwa wanaosakwa kumrithi Valverde huku ikidaiwa kwamba Koeman naye amegomea mpango huo.

Mkataba wa Valverde unakwisha mwisho wa msimu huu.