Wright: Sancho akitua tu, mbona Man Utd wanabeba

Monday June 29 2020
sancho1 pic

London, England. GWIJI wa zamani wa Arsenal, Ian Wright anaamini kwamba, Manchester United imeanza kurejea kwenye kiwango chake cha zamani.

Amesema viwango vya juu vinavyoonyeshwa na mastaa wake Bruno Fernandes, Paul Pogba, Anthony Martial na Marcus Rashford vimewafanya wababe hao kuwa bora zaidi uwanjani.

Hata hivyo, Wright ambaye amecheza kwa mafanikio makubwa wakati huo Arsenal ikiwa chini ya Arsene Wenger, alisema kuna mtu mmoja ambaye Man United wanapaswa kumnasa fasta ili kuwa watamu zaidi na kuwania mataji mbele ya Liverpool na Manchester City.

“Kwa sasa kila mtu anakunwa na ubora wa Fernandes, Pogba na Rashford uwanjani. Nadhani Manchester United wanarudi kwenye ule ubora wao kama wakati wa Ferguson (Sir Alex) na kushinda mataji. Lakini, wataongeza ushindani zaidi kama watamnasa Sancho (Jadon),” alisema Wright.

Alisema amekuwa akiifuatilia Man United namna inavyocheza na kubaini kuwepo na tofauti kubwa na sasa iko tayari kwa ushindani dhidi ya Liverpool na Manchester City kama itaongeza wachezaji wachache kwenye maeneo muhimu.

“Inashtua kwa kweli, angalia Fernandes na Pogba wanavyocheza pamoja ama Martial na Rashford na aina ya mabao wanayofunga uwanjani.

Advertisement

“Mara ya mwisho kuiona Manchester United kama hii ya sasa ni wakati ule walipokuwa na Chicharito [Javier Hernandez] na Dimitar Berbatov. Na sasa naona inakwenda kutokea kama wakati ule,” alisema Wright wakati akichambua mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA kati ya Norwich City na Man United.

United ilishinda mchezo huo kwa mabao 2-1 ndani ya dakika 120 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.

United haijashinda taji la EPL tangu msimu wa 2012-13.

Advertisement