Walioifunga Southampton warudisha chenji

Tuesday January 14 2020

 

LONDON ENGLAND. UNAAMBIWA hivi walioitesa Southampton mzunguko wa kwanza Ligi Kuu England sasa mmojammoja wanaanza kurudisha chenji. Jumamosi iliyopita, Southampton wakiwa ugenini huko King Power waliichapa Leicester City 2-1, staa wao Danny Ings akifanya mambo yake kupiga bao la ushindi huku wakiendeleza moto wao wa kuvishushia vichapo timu zote zilizowafunga kwenye mzunguko wa kwanza. Tayari wababe hao wamezichapa timu tatu zilizowatesa kwenye mzunguko wa kwanza. Kwenye duru la kwanza katika Ligi Kuu England, Southampton ilichapwa nyumbani 3-0 dhidi ya Chelsea, 2-0 dhidi ya Tottenham na 9-0 dhidi ya Leicester City.

Wakati hao wamegeuza kibao na kwenda kushinda ugenini dhidi ya timu hizo, ambapo waliianza kwa kuipiga Chelsea 2-0 uwanjani Stamford Bridge, kisha wakaichapa 2-1 Tottenham huko kwao London na kumalizia wikiendi iliyopita kwa kuwapiga 2-1 Leicester City uwanjani King Power na kuwafanya waenguliwe kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England. Southampton sasa inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo ikivuna pointi 28 katika mechi 22, ambapo wameshinda nane, sare nne na vichapo 10 huku wakiwa na mabao ya kufunga 27 na kufungwa 39.

Advertisement