Viwanja vya Magufului vyamuibua Akhwari

UNAMKUMBUKA John Stephen Akhwari? Kama umepitiwa, basi huyu ni mwanariadha mkongwe mwenye historia ya kusisimua, ambaye alimaliza mbio huku akiwa amefungwa bandeji kwenye Olimpiki.

Sasa buana, Akhwari ameamua kuvunja ukimya baada ya wachezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars) na bondia Hassan Mwakinyo kuzawadiwa viwanja na Rais John Magufuli hivi karibuni.

Stars walizawadiwa viwanja hivyo vya mjini Dodoma na Rais Magufuli baada ya kufuzu kucheza Afcon 2019 sanjari na bondia Hassan Mwakinyo ambaye alianza kuvuma mwaka jana baada ya kumchapa Samm Eggington wa Uingereza.

Hamasa hiyo ya Rais kwa nyota hao imemuibua Akhwari aliyesema ingekuwa enzi zao kila mwaka wangezawadiwa.

“Riadha tunafanya vizuri, lakini sikumbuki kama tumewahi kuzawadiwa, ila nafikiri ni sababu riadha si watu wa kupiga kelele kujitangaza sana, lakini katika mafanikio ya kimichezo tunaongoza mpaka sasa.”

Mwanariadha huyo ambaye alikuwa maarufu kwenye Olimpiki ya 1968 kule Mexico na Tanzania ilishiriki kwa mara ya pili baada ya ile ya 1964 wakati huo ikijulikana kama Tanganyika anakwambia, soka wanajua kujipamba ndio sababu wanapewa kipaumbele.

“Riadha tunafanya vizuri, lakini hatujui kujipamba ili tuonekane, nadhani siku ikitokea soka wamefuzu kucheza Olimpiki, itakuwa ni ‘big issue’, lakini riadha kila msimu wanafuzu olimpiki inachukuliwa kawaida.”