Uzoefu unaitesa Tanzania, Kenya Burundi AFCON

Monday June 24 2019

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Wazungu hawakukosea waliposema 'experience is a good teacher' msemo ambao kwa lugha hadhimu ya Kiswahili unatafsiriwa kama uzoefu ni mwalimu mzuri wenye lengo la kuonyesha faida na umuhimu wa uzoefu wa mtu juu ya jambo fulani.

Mwanzo usio mzuri kwa timu tatu kutoka Afrika Mashariki kati ya nne zinazoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea huko Misri ni ishara tosha ya namna gani uzoefu ulivyo na maana kubwa kwenye mchezo wa mpira wa miguu kokote duniani.

Ukiondoa Uganda iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya DR Congo, Burundi ilijikuta ikichapwa bao 1-0 na Nigeria, Tanzania 'Taifa Stars' ikatandikwa 2-0 na Senegal wakati Kenya ilichapwa 2-0 na Algeria.

Ni uzoefu ambao uliitofautisha Uganda na ndugu zake watatu kutoka Afrika Mashariki kiasi cha kupata ushindi dhidi ya DR Congo ambayo imesheheni idadi kubwa ya wachezaji wenye majina makubwa na wanaotamba kwenye klabu mbalimbali Ulaya.

Kwenye mchezo wao dhidi ya DR Congo, wachezaji wa Uganda walicheza kwa utulivu wa hali ya juu, walionyesha nidhamu ya mbinu, lakini hawakufanya makosa makubwa ambayo yangeweza kuwapa mwanya wapinzani wao kupata nafasi ya kutumbukiza mpira langoni mwao.

Uganda ilionekana ni tishio katika kutumia kila nafasi waliyoitengeneza jambo lililoiweka safu ya ulinzi ya DR Congo matatani, lakini hata pale waliposhambuliwa kila mmoja alitimiza vyema jukumu la kuusaka mpira.

Advertisement

Kwa bahati mbaya kile ambacho kilioonyeshwa na hatukuweza kukiona kwa Kenya, Burundi na Tanzania. Pamoja na Burundi na Kenya kucheza vizuri kwenye mechi zao, wachezaji wao walipoteza umakini na kujikuta zikipoteza mechi zao huku Tanzania ikikosi nidhamu ya mbinu kwa wachezaji sambamba na kufanya makosa ya mara kwa mara ambayo yaliigharimu.

Uzoefu ambao Uganda waliupata kwa kushiriki fainali hizo awamu iliyopita umewasaidia kwa kuwafanya watambue namna ya kuyacheza tofauti na Kenya iliyoshiriki kwa mara ya mwisho mwaka 2014, Tanzania iliyoshiriki mwaka 1980 na Burundi ambayo haijawahi kushiriki kabisa.

 

Vigogo vijipange

Ni wazi kwamba zipo timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kufanya vyema na ikibidi kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kama vile Senegal, Ivory Coast, Nigeria, Cameroon, Misri, Morocco na Ghana lakini kwa kiwango na ubora wa soka ulioonyeshwa kwenye mechi za kwanza na baadhi ya timu ambazo hazipewi nafasi, vinapaswa kuviamsha vigogo hivyo.

Pamoja na kupoteza mechi za kwanza, Namibia, Zimbabwe, Burundi zilionyesha ubora wa hali ya juu licha ya kupoteza mechi wakati Madagascar inayoshiriki kwa mara ya kwanza iliweza kuibana Guinea na kutoka nayo sare ya mabao 2-2 huku ikionyesha kiwango bora.

Kama timu hizo zenye majina makubwa zisipojipanga vyema, fainali za AFCON mwaka huu zinaweza kuleta bingwa ambaye wengi hawamtarajii.

Misri imetendea haki mashindano

Ikiwa ndio kwanza hatua ya makundi ya fainali za AFCON imeanza, waandaaji wa mashindano hayo mwaka huu, Misri wanastahili pongezi za hali ya juu kwa namna walivyoyafanya yawe na mvuto wa hali ya juu kutokana na namna walivyo na mpangilio mzuri na uwekezaji walioufanya katika kuziandaa.

Viwanja vinavyotumika vina ubora na hadhi ya hali ya juu, sherehe za ufunguzi zilikuwa na mvuto wa kipekee na hakujareipotiwa matukio ya usumbufu kwa wageni na timu shiriki.

Mastaa gani kuibuka?

Fainali za AFCON kila zinapofanyika zimekuwa zikiibua mastaa ambao hunufaika nayo kwa kupata fursa ya kuzitoa udenda klabu mbalimbali kubwa duniani.

Kuanzia kwa akina Salomon Olembe, Rigobert Song, Shaun Bartlett, Julius Aghahowa hadi akina Ahmed Hossam 'Mido', Mohamed Nagy 'Gedo', Junior Kabananga na Alain Traore wote walinufaika kutokana na mashindano hayo.

Kwa aina ya ushindani ambao timu zimeanza kuonyesha, ni nwazi kwamba AFCON ya mwaka huu itatuibulia nyota wengine wapya kama ilivyofanya hapo nyuma.

Advertisement