Uefa kupigwa ngumi jiwe!

Sunday May 31 2020

 

SEVILLE HISPANIA. SIKIA hii. Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limeripotiwa kuwa na mpango wa kuzifanya mechi za kuanzia hatua ya robo fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League msimu huu kupigwa moja tu huku zikifanyika katika kituo kimoja.

Michuano hiyo yote imesimamishwa kutokana na janga la corona, ambapo fainali zake zilipangwa kufanyika kwenye miji ya Istanbul na Gdansk zimeahirishwa pia.

Hata hivyo, mpango wa Uefa ni kufanya michuano hiyo kumalizika Agosti baada ya michuano ya ligi za ndani kufika tamati.

Jiji la Lisbon la Ureno au miji ya Ujerumani imedaiwa kwamba huenda ikachaguliwa kuwa kituo cha michuano hiyo ya Ulaya kwa kuanzia raundi inayofuatia.

Rais wa klabu ya Getafe, Angel Torres alithibitisha kwamba UEFA ina mpango huo wa kucheza mechi zote zilizobaki kwenye michuano yake ya Ulaya msimu huu kwenye jiji moja, huku mechi za robo fainali na nusu fainali zikipigwa moja moja tu tofauti na ule mfumo uliozoeleka wa mechi mbili.

“Wazo la UEFA ni Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League, kuanzia hatua ya robo fainali ichezwe mechi moja katika uwanja mmoja licha ya kwamba hilo halijathibitishwa bado,” alisema Torres.

Advertisement

“Watafanya uamuzi hiyo Juni 17 wakati wa mkutano wa kamati kuu utakapoketi.”

Getafe mechi yao ya kwanza dhidi ya Inter Milan iliahirishwa baada ya Torres kutishia kugomea mechi hiyo kama Uefa hawataingilia kati kufuatia mahali ilikopaswa kufanyika, Italia kulikuwa kumeathirika zaidi na janga la corona.

Advertisement