Timu 15 hatarini kushuka Ligi Kuu

Monday June 29 2020
timu pic

Dar es Salaam. Wakati timu ya Singida United ikiwa ya kwanza kushuka daraja, timu nyingine 15 ziko hatarini kuifuata timu hiyo.

Ingawa Mbao, Mbeya City na Ndanda ziko hatarini zaidi lakini Alliance (36), KMC, Lipuli na Mtibwa zenye pointi 37 kila moja kama hazitachanga karata zao vema kwenye mechi zao sita zilizosalia kuna uwezekano zikaungana na Singida.

Nyingine ni Mwadui (40), Ruvu Shooting na Tanzania Prisons zenye pointi 43 kila moja, Biashara United (44), Kagera Sugar (45), JKT Tanzania na Polisi Tanzania zenye pointi 47 kila moja.

Sanjari na Coastal Union yenye pointi 48 ambazo licha ya kutokuwa katika hatari zaidi, bado ziko kwenye mstari wa kushuka daraja kama zitapoteza mechi zao zote na Mbao, Mbeya City na Ndanda zikashinda mechi zote.

Hadi sasa timu zenye pointi 53 au zaidi katika msimamo ndizo ziko salama, ambazo ni Simba (79), Yanga (60), Azam (59)na Namungo yenye pointi 56 huku Coastal Union iliyo katika nafasi ya tano ikihitaji ushindi katika mechi mbili ili kuwa salama zaidi, vivyo hivyo kwa timu zilizo chini yake.

Kama Mbao ambayo ni ya pili kutoka mwisho, itashinda mechi zote zilizosalia ikiwamo ya jana iliyowachapa Polisi Tanzania 1-0, itafikisha pointi 47, Mbeya City 51 na Ndanda 53 huku zikiombea mabaya kwa timu tatu zilizo juu yake zifungwe mechi zao zote ili zijinasue.

Advertisement

Msimu huu timu nne zitashuka moja kwa moja huku mbili zikicheza hatua ya mtoano pamoja na timu za Ligi Daraja la Kwanza. Tayari Singida imeshuka baada ya kufungwa mechi 23, kutoka sare mechi 6 na kushinda michezo mitatu licha ya kuwa ina mechi sita mkononi.

Akizungumzia matokeo hayo, kocha msaidizi Zulkifri Mahad alisema yametokana na kukosa ushirikiano.

“Timu kufanya vizuri au vibaya kuna mambo mengi, ila kikubwa ni ushirikiano kati wachezaji, benchi la ufundi, wadau na uongozi,” alisema.

Alisema licha ya Singida kushuka daraja, mchezaji na kocha wataendelea kuwepo na sasa kila mmoja anawaza maisha mengine ya kisoka.

“Ikitokea Singida ikawa vizuri, basi wapo wanaoweza kubaki na kupambana tena ili kuipandisha.”

Singida United itakuja Dar es Salaam kucheza na Azam, KMC, Yanga na Ruvu Shooting (Pwani) kabla ya kurudi Singida kucheza na Kagera Sugar na Biashara United mechi zake za kuhitimisha ratiba.

Advertisement