Tatizo sio hawa kina Kagere, Wazawa ndo hawajielewi tu!

Monday June 24 2019

 

By BADRU KIMWAGA

TAIFA Stars imeyumba kwa miaka kadhaa. Ni mwaka huu ndio tumeweza kufuzu fainali za Afcon 2019 na usiku wa leo itatupa karata yao ya kwanza dhidi ya Senegal katika mechi za Kundi C ambalo pia lina Algeria na Kenya zitakazovaana pia usiku wa leo.

Timu yetu ya Taifa kwa miaka mingi ilishindwa kufanya vizuri na hata miaka ya karibuni imekuwa ikiyumba kwenye mashindano makubwa. Stars imekuwa ya kawaida sana wala si tishio tena kama enzi za nyuma.

Tumefuzu Misri kama zali tu kwa sababu Lesotho walioshindwa kufuzu, walizoa alama nne kwa Stars. Ni timu ya kawaida sana, lakini walitubana nyumbani na kupata sare ya 1-1 kisha kwenda kutufungwa kwao. Cape Verde walitufunga kwao na kuja kulipa kisasi nyumbani, Uganda wao tumevuna alama nne kwao, moja mjini Kampala kisha kuja kuwafunga wakiwa tayari wameshafuzu. Hatuwezi kujisifu sana, hata kama ni kweli tupo Misri.

Nieleweke mapema, mi ni mmoja wa wadau wanaoiombea Stars ifanye maajabu Misri licha ya kupenya kwa zali. Bahati huwa haiji mara mbili, tumeipata baada ya miaka 39, kwa nini tusiitumie?

Kukwama kwa Stars kwa miaka hiyo 39 na kupata zali mwaka huu kumekuwa kukielezwa na kuzungumzwa na wadau ni uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni kwenye timu kubwa za Simba, Yanga na Azam ndiyo tatizo.

Hata wikiendi iliyopita Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alisema. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe naye alikazia na kutangaza kabisa huenda msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, idadi ya nyota wa kigeni wa kucheza mechi moja itapunguzwa. Badala ya kucheza wote 10 waliosajiliwa na klabu moja ambao waliruhusiwa kucheza mchezo mmoja, sasa itakuwa ni watano tu.

Advertisement

Hoja za wote na wadau wengine ni, wageni wanapewa zaidi nafasi kwenye hizo timu kuliko wazawa hasa kwenye ulinzi na ushambuliaji. Ukienda pale Azam kulikuwa na kina Yakub Mohammed, Nicholas Wadada, Bruce Kangwa, Stephen Kingue, Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Enock Atta Agyei na Daniel Amoah.

Yanga katika beki tangu aondoke kina Vincent Bossou, ulinzi wao ulilindwa na wazalendo, ila kati na kule mbele kulikuwa na Papy Kabamba Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe na Heritier Makambo.

Msimbazi ndio kulikuwa funga kazi, walikuwa na Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Zana Coulibaly, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere. Yaani ukimtoa Aishi Manula tu ambaye ni kipa, Simba ilikuwa inaweza kuchezesha nyota wote wa kigeni katika mchezo mmoja freshi bila tatizo kuanzia beki namba mbili hadi mshambuliaji namba 11. Asilimia kubwa walikuwa wana jezi za kikosi cha kwanza waswahili wako benchi wanasubiri nje! Ukiangalia tatizo utarudi kulekule wazawa wanazidiwa uwezo na wageni tutake tusitake. Asilimia kubwa ya wazawa hawana nidhamu ya mchezo pia wavivu wa mazoezi.

Hapo hatutaji suala la majeruhi wa mara kwa mara na visingizio vingine kibao.Wachezaji wetu wanachukulia soka kirahisi sana na ndio maana hawa makocha kwenye hizi timu kubwa wanaishia kutumia wageni ambao wako tayari kwa kazi, kwa vile na wao wanataka ushindi na wanaangalia usalama wa ajira zao. Wao ishu ya Taifa Stars haiwahusu, wala si jukumu la klabu kuitengeneza Stars. Klabu ina malengo yake. Zinataka kutengeneza faida kupitia ushindi, hivyo lazima itafute watu wa kuutengeneza huo ushindi ndio hao kina Wawa, Kagere, Chama sasa, haijalishi kwamba Yusuf Mlipili, Hassan Dilunga ama Adam Salamba watakaa benchi au jukwaani.

Wenzetu wanaweza kuwa wana umri mkubwa, lakini wanajua maana ya nidhamu ya mpira, huwezi kumkuta anafanya masihara na mazoezi wala kuzingua uwanjani. Kila kitu kina wakati wake na ndio kinachotushinda waswahili.

Ukifanya tathmini ndogo tu utaona wachezaji wetu wanapotea ndani ya muda mfupi sana kuliko ilivyo ligi za nchi zote jirani. Mastaa wengi wazawa wanacheza muda mfupi sana kabla ya kujilazimisha au kulazimishwa kustaafu kutokana na uhalisia wa klabu zetu na kutojielewa kwa wachezaji binafsi.

Ukifanya tathmini ya haraka utagundua wachezaji waliocheza Ligi ya Bara kwa kipindi kirefu hawafiki hata kumi na hata hao wenyewe viwango vyao vimekuwa vya kawaida sana. Yupo Shabaan Nditi wa Mtibwa, Juma Kaseja wa KMC, Kelvin Yondani wa Yanga, John Bocco, George Kavila wa Kagera na wengine wachache.

Lakini Nditi ndiye aliyecheza kwa miaka zaidi ya kumi mfululizo kwani hao wengi wamekuwa wakiacha na kurudi wanavyojisikia. Ukiangalia katika nchi jirani hata DR Congo utagundua wachezaji wengi wanacheza misimu mingi na hawachuji kuanzia kwenye klabu mpaka timu za Taifa. Meddie Kagere licha ya kuwa na umri mkubwa, lakini anaendelea kusumbua nchini. Msimu uliopita ukiwa wa kwanza kwake kucheza Tanzania kawakimbiza wazawa kibao na kuchukua kiatu cha dhahabu kwa kufunga mabao 23. Kabla ya hapo Okwi ambaye naye alikuwa akitajwa kibabu aliwakimbiza kina Ibrahim Ajibu, John Bocco, Said Dilunga, Juma Javu na wengineo.

Bila kuuheshimu mpira ni ngumu kufanikiwa kwa vile soka lina miiko yake, wachezaji wanapaswa kujituma na kujilinda kiafya na kiakili. Tusikimbilie tu kunyooshea vidole wageni ndiyo wametuvurugia ligi, tuangalie je wazawa akili zao zikoje? Wanafahamu kile wanachokifanya?

Wachezaji wazawa wanapaswa kujitathmini sana na ifike mahali hata klabu pia ziwasaidie kwa ushauri na akili, ili ziwatumie muda mrefu na wanufaike nao pia kuibeba Stars yetu.

Kufa kwa viwango vya wachezaji ndani muda mfupi kunaingiza klabu kwenye gharama za kufanya usajili mpya jambo ambalo linaweza kuepukika kama wakiweka miundombinu mizuri hata ya kuangalia afya zao mara kwa mara na hii ni pamoja na aina ya vyakula wanavyokula.

Huwezi kugonga chipsi mayai na wale kuku wa dawa, ukaongezea na ulabu tu, kisha ukajirusha na vimwana halafu unataka kuwa mchezaji imara. Huko ni kujidanganya tu.

Tusiwalaumu hawa kina Kagere, Chirwa, Ngoma na Wawa au Kangwa, wachezaji wetu hatujawalea kisoka. Tukumbuke ni klabu tatu tu kati ya 20 ndizo zenye kusajili nyota wa kigeni na kuwatumia kwa wingi na kuzipa matokeo, wale wazawa zaidi ya 500 waliopo timu nyingine 17 wanafanya nini? Kwa nini hawatambi na kuonwa na makocha wa timu ya Taifa?

Advertisement