TIGERE fundi mwingine pale Azam FC

Sunday May 17 2020

 

By THOMAS NG’ITU

MPIRA wa Tanzania unazidi kuchanua na kufanya nchi yetu ianze kutambulika kile pembe ya bara hili na nje baada ya wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kuja nchini.

Hali hii ya mastaa wa kigeni kufurika Tanzania ilianza kukolea mwanzoni mwa miaka ya 2000 lakini kadri muda ulivyozidi kwenda mambo yakazidi kuongezeka ubora.

Sasa wachezaji wa kigeni wapo kwa wingi zaidi nchini na mamlaka husika zimeamua kuweka vigingi ili kuhakikisha wanaokuwepo au wanaokuja ni wale bora zaidi wanaocheza kwenye timu zao za Taifa.

Katika kikosi cha Azam dirisha dogo la usajili walimsajili kiungo matata kutoka katika klabu ya FC Platinum inayoshiriki Ligi Kuu nchini Zimbabwe. Anaitwa Never Tigere.

Mwanaspoti ilifanya naye mazungumzo namna alivyopata dili hilo na kusajiliwa na Azam FC na maisha anavyoyaona hapa nchini.

Mwanaspoti: Mambo vipi kaka, hongera kwa kuja Tanzania?

Advertisement

Tigere: Ahsante sana kaka, Nashukuru kuwa hapa ni sehemu nzuri sana kwa kazi yetu.

Mwanaspoti: Ilikuaje mpaka ukafika hapa Azam FC na uliijuaje Ligi Kuu ya Bara?

Tigere: Aisee Bosi yule CEO wa Azam (Abdulkarim Amin ‘Popat’) aliniona mimi nikicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa kule Misri dhidi ya Al Ahly ndio akaniambiwa kwamba ananihitaji katika kikosi chao, mambo yakaanza mpaka yakamalizika nikaja.

Mwanaspoti: Kwanini ikawa rahisi kwako kukubali wewe kuja huku moja kwa moja?

Tigere: Unajua kila mtu anapenda mazingira mazuri, kwahiyo Azam ni sehemu nzuri kwangu na ina vitu ambavyo mwanasoka yeyote wa Kiafrika angependa kuwa navyo au kuhusishwa navyo.

Mwanaspoti: Tofauti ya soka la hapa na kwenu Zimbabwe ni ipi?

Tigere: Hakuna tofauti kubwa japo ni kwenye namna ya msimu wa Ligi unavyoanza, Ligi ya Zimbabwe inaanza mapema mwanzo wa mwaka wakati Ligi ya hapa inaanza katikati ya mwaka, lakini inabidi nizoee mazingira. Ndio kazi yetu, soka ni lilelile tu.

Mwanaspoti: Katika kikosi chenu kuna changamoto kwenye eneo la kiungo, unacheza na Sure Boy, Masoud Abdallah na wengineo wewe hili unalikabilije?

Tigere: Kweli kuna changamoto kubwa lakini inabidi niizoee, hata nilivyokuwa Platinumz ilikuwa hivi hivi. Sehemu yoyote penye changamoto ndipo mtu unaweza kukua kisoka.

Mwanaspoti: Kitu gani ambacho kinakupa changamoto tangu uwasili nchini?

Tigere: Mhh hali ya hewa ya joto lakini nimeshaanza kuizoea, lakini kingine ni lugha ambapo na mimi nimeanza kujifunza na naamini kila kitu kitakuwa sawa ndani ya muda mfupi.

Mwanaspoti: Malengo yako ni nini ukiwa na Azam?

Tigere: Nataka kuifungia magoli zaidi Azam ili niweze kupata mkataba mwingine wa kuendelea kubaki hapa kwavile ni sehemu nzuri na mchezaji unaweza kupata nafasi ya kukua kisoka ndani na nje ya uwanja.

UBORA WAKE

Tigere ni mzuri katika kupiga pasi fupi na ndefu, mzuri katika kupiga mipira iliyokufa (frii-kiki) na pia ni mzuri katika kuanzisha mashambulizi.

Mwaka 2019 akiwa na FC Platinum alikuwa ni nyota wa mwaka katika kikosi hicho na mwaka 2016 wakati anaichezea Kariba FC alikuwa mfungaji bora wa klabu hiyo.

Mafanikio hayo ni kati ya vitu vinavyomfanya aamini kwamba anaweza kufanya makubwa Azam.

Anatamani kuisaidia timu hiyo iliyopanda daraja msimu wa 2008-09 itwae ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya pili baada ya kulibeba 2013–14.

Advertisement