Simba yarejea Dar kimya

Dar es Salaam. Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba wamerejea jijini hapa jana mchana bila mbwembwe wala shamrashamra wakitokea jijini Mbeya ambako walifanikiwa kutetea taji hilo baada ya kuvuna pointi nne katika mechi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prison.

Baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), wachezaji na viongozi wa timu hiyo waliunganisha safari yao kuelekea kambini kujiandaa kwa mechi ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Azam FC kesho.

Tofauti na ilivyozoeleka, timu zinapopata mafanikio nje ya mkoa huu, kikosi cha Simba kilipowasili, hapakuwa na mashabiki walioilaki na kuipa shangwe baada ya kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo.

Kocha wa Simba, Sven Vandenvroeck alisema kutwaa ubingwa lilikuwa jambo kubwa na la furaha kuanzia benchi la ufundi, wachezaji, viongozi, mashabiki na watu wengine wote ambao wanahusika na timu yao kwa namna moja au nyingine.

“Tumekamilisha hili la ligi kwa maana ya kutwaa ubingwa na jukumu lingine kubwa ambalo lipo mbele yetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika Kombe la FA, tuhakikishe tunachukua ubingwa mwingine na kuweka historia kubwa,” alisema.

“Leo (jana) tutafanya mazoezi mepesi jioni na kesho (leo)ndipo tutafanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mechi. Uzuri wachezaji wangu wote wapo fiti na kazi itabaki kwangu kuchagua wale ambao nitataka kuwatumia katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Azam.”

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema matokeo waliyopata katika mechi hizo za Mbeya yamebaki historia ya furaha kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa na sasa akili ya wachezaji wote ipo katika mchezo unaofuata.

Beki wa timu hiyo, Erasto Nyoni ambaye kama Bocco alitua Simba akitokea Azam alisema siri ya kutwaa ubingwa ni umoja, mshikamano na ushirikiano walionao.

Ofisa mtendaji mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema baada ya ubingwa ambao ulikuwa lengo kuu, akili, nguvu na maandalizi yanahamia mechi dhidi ya Azam.

Alisema maandalizi yameanza mara moja kwa uongozi kuwapatia wachezaji na benchi la ufundi mahitaji ya msingi ikiwamo motisha kama watashinda mechi hiyo.

Azam yatia neno

Azam kwa upande wake, imeipongeza Simba kwa kutwaa taji hilo huku kiwataka waamuzi wa Ligi Kuu kuchezesha bila makandokando katika msimu ujao ili bingwa apatikane bila manung’uniko.

Akizungumza jijini hapa jana, Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka’ alisema kumekuwa na malalamiko mengi katika baadhi ya mechi za timu yake akidai kwamba kitendo hicho kinapoteza sifa halisi ya ubingwa.

Alisema bingwa anatakiwa kupatikana bila ya kuwa na dosari kama zilizojitokeza katika msimu huu.

“Hongera yao lakini ubingwa unapoutwaa huku kukiwa na malalamiko juu ya mechi zako unakuwa haupendezi, hivyo waamuzi msimu ujao wajitahidi kuwa makini na kuchezesha kwa haki ili bingwa apatikane bila malalamiko, ashinde mechi zake kihalali, pia wasimamizi wa soka waliangalie hilo,” alisema.

Zaka alisema Azam imeukosa ubingwa wa Ligi Kuu ambao ulikuwa moja ya malengo yake na kwamba inajipanga kuwa na kikosi bora kitakacholeta ushindani msimu ujao.

Alisema wamesahau yaliyotokea Kagera walipoumana na Kagera Sugar na kukubali kipigo cha bao 1-0 pamoja na sare ya bao 1-1 waliyopata katika mchezo dhidi ya biashara na sasa akili ipo katika mchezo wa FA dhidi ya Simba.

Alisema mchezo huo ndio utakaoibakiza katika kuwania kikombe kwani ndicho kilichosalia, “makombe mengine tumeshayakosa, lililobaki ni hili la FA basi, Jumatano (kesho) utakuwa mchezo wa ushindani, tunahitaji nafasi hiyo ili mwakani tupate uwakilishi katika michuano ya kimataifa,” alisema.