Simba wametwaa taji la 21 Bara

Muktasari:

  • Wekundu wa Msimbazi wametwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1980.

Mbeya. Wekundu wa Msimbazi Simba jana waliandika historia baada ya miaka 40 kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo.

Taji hilo la 21 kwa Simba katika ligi hiyo tangu mwaka 1965 ililipata baada ya kutoka suluhu na Tanzania Prisons lililopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Sare hiyo ya bila ya mabao imeifanya Simba ifikishe pointi 79, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote huku zikiwa zimesalia mechi za raundi sita kabla ya kumalizika kwa msimu.

Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kubeba taji mara tatu mfululizo tangu ilipobeba mara ya mwisho ubingwa huo mara tano mfululizo kuanzia 1976 hadi 1980.

Katika mchezo huo uliokuwa na upinzani wa aina yake kuanzia mwanzo hadi mwisho, Simba ilianza na kikosi kilichokuwa na mabadiliko makubwa baada ya nyota wake saba wa kikosi cha kwanza kuanzia benchi.

Wachezaji hao ni Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Francis Kahata, Pascal Wawa, John Bocco, Luis Jose Miquissone na Clatous Chama.

Simba iliingia katika mchezo huo kwa nidhamu kubwa ya kushambulia na kuzuia kwa kuanza na mfumo wa 4-3-3, ulioiwezesha kucheza kiushindani hasa eneo la kiungo.

Katika eneo hilo Simba ilianza na Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga na Gerson Fraga wakati Prisons ikiwa na Ezekiel Mwashilindi, Jumanne Nkazi na Adilly Buha ambao walikuwa wakishindana kwa matumizi ya nguvu na akili.

Ukiondoa ushindani huo ulikuwa katika eneo la kiungo Simba pia ilifanya mabadiliko katika safu ya ulinzi ikiwacheza Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Haruna Shamte na Gadiel Michael walikuwa na nidhamu kubwa katika kuzuia washambuliaji wa Prisons, Jeremia Juma, Salum Kimenya na Samson Mbangula.

Kama kina Mbangula wangekuwa makini wangeweza kuifungia timu yao mabao kwani walitengeneza nafasi nyingi kuliko Simba lakini juhudi zao ziliishia mikononi mwa kipa Aishi Manula au kutoka nje ya lango.

Prisons iliyotawala mchezo huo kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Simba, ilionekana dhahiri kusaka ushindi baada ya mechi yao ya raundi ya kwanza jijini Dar es Salaam kumalizika pia kwa sare ya 0-0.

Kocha wa Prisons, Mohammed Rishard ‘Adolf’, alionekana kuwapa maelekezo vijana wake kuhakikisha washambuliaji watatu wa Simba, Ibrahim Ajib, Meddie Kagere na Miraj Athuman hawapati nafasi ya kumiliki mpira katika eneo la lango lao huku kipa wao, Jeremiah Kisubi akifanya kazi ya ziada mara kadhaa kuokoa hatari zilizoelekezwa langoni kwake.

Licha ya timu zote kushambuliana kwa zamu na kufanya kosa kosa nyingi pambano liliisha bila ya mabao na wachezaji wa Simba na maafisa wao walionekana kupongezana bila ya mashamsham.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara aliwaamsha mashabiki jukwaani baada ya kuingia ndani ya dimba la kuchezea na kushangia kwa kunengua huku akiungwa mkono na mashabiki walioshuka kutoka majukwaani.

Wachezaji wa Simba baadaye walionekana wakishangilia wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na baadaye wakiwa kwenye gari lao wakati wakielekea kwenye kambi yao iliyopo pembeni ya jiji huku mashabiki wakitapakaa barabarani kuusindikiza msafara wa timu hiyo inayowasili asubuhi hii ili kujiandaa na mechi yao ya Kombe la ASFC dhidi ya Azam Jumatano.