Simba,Yanga utamu upo hapa!

DROO ya michezo ya robo fainali ya michuano ya Azam Sport Federation (ASFC) ilichezweshwa juzi Ijumaa huku vigogo wote wa Ligi Kuu wakijikuta kwenye mtihani mkubwa.

Michezo hiyo itakuwa ya kulipa visasi kwa baadhi ya timu baada ya kuambulia vichapo kutoka kwa wapinzani wao katika michezo ya Ligi Kuu walipokutana msimu huu.

Pia tangu michuano hiyo iliporudishwa kwa mara nyingine msimu wa 2015/2016, hakuna timu iliyowahi kubeba mara mbili, hivyo inafungua nafasi kwa Azam FC, Yanga na Simba kulibeba kwa mara ya pili kama watafanikiwa na kuandika rekodi.

Yanga walikuwa wa kwanza kulinyakua kombe msimu wa mwaka 2015/16, Simba nayo ikabeba uliofuata, Mtibwa Sugar imelinyakua pia na msimu uliopita Azam FC ikalibeba kombe kwa kuifunga 1-0 Lipuli FC. Katika michezo ya robo fainali Simba itaikaribisha Azam FC ambao ni mabingwa watetezi huku ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa michezo yote miwili ya Ligi Kuu msimu huu.

Mchezo wa kwanza timu hizo zilikutana Oktoba 24 katika Uwanja wa Taifa na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Meddie Kagere dakika ya 48, na mchezo wa marudiano Azam ilichapwa 3-2 kwa mabao ya Erasto Nyoni, Deo Kanda na Kagere huku yale ya Azam yakifungwa na Never Tigere na Idd Seleman ‘Nado’.

Kwa upande wa Yanga ambao watakutana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu wamekutana mara moja na Yanga kulala 3-0 Uwanja wa Uhuru, Januari 15, mwaka huu.

Mabao ya Mtibwa inayonolewa na Mecky Maxime yalifungwa na Yusufu Mhilu, Ally Ramadhan Peter Mwalyanzi ikiwa ni siku chache baada ya timu hizo kutoka kwenye Kombe la Mapinduzi, Zanzibar.

Namungo FC watacheza na Alliance FC ambao kwenye Ligi Kuu wamekutana mara moja na kutoshana nguvu ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Majaliwa yaliyofungwa na Reliants Lusajo (Namungo) na Zabona Hamis (Alliance).

Sahare All Stars ya Tanga inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ndio timu pekee ya ligi daraja la chini iliyosalia kwenye kombe hilo baada ya kuichapa 5-2 Panama FC ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL), kabla ya hapo iliichapa Mtibwa Sugar kwa penalti 3-2 baada ya sare ya bao 1-1.

Sahare inayoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Kundi B ikiwa na alama 19 inakutana na Ndanda FC inayoshika nafasi ya 16 ikiwa na alama 31 kwenye Ligi Kuu.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Kagera, Mecky Maxime alisema utakuwa mchezo mgumu kwa kila timu kutokana na kila moja kuutaka ubingwa.

Kocha wa Sahare, Abdallah Kessy alisema licha timu hiyo kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja lakini lengo lao ni kufika fainali ya FA na kuandika rekodi ya kipekee.

“Timu zote ni nzuri na bora zilizoingia hatua hiyo, hivyo hakuna timu ambayo mtu anaweza kusema mbovu kwani imefanya juhudi na kufika hatua hiyo.

“Kinachosaidia FA inakuwa ‘live’ ndio maana tumefika hapa tulipo na tuna uwezo wa kucheza na timu yoyote ile na lengo letu ni kufika fainali,” alisema Kessy.

Kocha msaidizi wa Alliance FC, Mathias Wandiba alisema haoni kitu cha kuwakwamisha kwenda nusu fainali kwa kuwa wamejipanga vyema hadi kufikia hatua hiyo.

“Mashindano ya FA yanachezwa kipekee sana ndio maana hakuna bingwa wa kujirudia tangu imerudi, hivyo yeyote anaweza akawa bingwa,” alisema Wandiba.