Samatta maji ya shingo Aston Villa

Monday June 29 2020

 

By MWANDISHI WETU

JAHAZI la chama la Mbwana Samatta la Aston Villa kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) linazidi kuzama baada ya Juni 27 kuchezea kichapo kingine ikiwa nyumbani kwa kugongwa bao 1-0 na Mbweha wa Birmingham, Wolverhampton.

Katika mchezo huo, nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars alianzishwa na kucheza kwa dakika zote 90 kwa mara ya kwanza tangu EPL ilivyorejea baada ya janga la corona, lakini mambo hayakuwa mazuri kwa chama lake kwa kupasuka huku wakijiona.

Villa wakiwa kwenye Uwanja wao wa Villa Park, walikuwa wakisaka pointi tatu za kuwatoa nafasi ya 19 na kuweka hai matumaini ya kusalia kwenye ligi hiyo kwa msimu ujao, lakini bao pekee la kipindi cha pili lililowekwa kimiani na Leander Dendoncker liliwanyong’onyesha.

Dondoncker alifunga bao hilo dakika ya 62 kwa shuti kali baada ya kupewa pasi na Jonny aliyekuwa ameanguka langoni mwa Villa kuipa timu yake pointi tatu muhimu zilizowapandisha kutoka nafasi ya sita hadi ya tano wakiishusha Man United.

Villa waliwabana wapinzani wao hao kwa dakika 45 za kwanza, lakini katika kipindi cha pili hasa baada ya kuingia kwa Adama Traore aliyechukua nafasi ya Diogo Jota katika dakika ya 60 ilichangamsha safu ya ushambuliaji wa Wolves na kusaidia kupatikana kwa bao hilo.

Villa waliosaliwa na mechi sita zikiwamo tatu dhidi ya vigogo, Man United, Arsenal na Liverpool waliokwishakutwaa ubingwa bila hata kushuka uwanjani baada ya kurahisishiwa kazi na Chelsea, wanatakiwa kuhakikisha washinde mechi hizo, vinginevyo wataiaga rasmi EPL kwa msimu ujao.

Advertisement

Advertisement