Kisa corona: Ronaldo, nyota wa Juventus wakatwa mishahara miezi minne

Muktasari:

Mapema mwezi huu familia ya Agnelli inayomiliki klabu ya Juventus ilichangia euro10 milioni katika kampeni za kupambana na corona nchini Italia.

Rome, Italia. Cristiano Ronaldo na wachezaji wenzake wa Juventus pamoja na kocha Maurizio Sarri wamekubaliana kukatwa mshahara wa miezi minne wa zaidi ya dola 100milioni ili kuisaidia klabu hiyo kutoyumba kiuchumi katika kipindi hiki cha janga la corona.

Klabu hiyo imesema fedha hizo za miezi minne zinauwezo wa kulipa mishahara kwa wachezaji watatu kwa mwaka.

Kwa mara ya kwanza kutokea makubaliano haya katika Serie A ikiwa ni wiki tatu tangu Ronaldo, mchezaji anayelipwa fedha nyingi zaidi katika Serie A kuamua kutoa zaidi ya dola 11 milioni.

Nahodha wa Juventus, Giorgio Chiellini mwenye digrii ya uchumi aliongoza majadiliano kati ya klabu na wachezaji wenzake.

''Mechi zilizobaki za msimu huu zitabadilika ratiba, klabu imefikia makubaliano na wachezaji pamoja na kocha kuangalia namna ya kulipwa fidia katika mechi za mwisho wa msimu,'' ilisema Juventus.

Wakiwa na lengo la kuendeleza rekodi ya kutwaa taji la tisa mfululizo la Serie A, Juventus inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja kwa Lazio.

''Juventus inapenda kuwashukuru wachezaji na kocha kwa uamuzi wako wa kuisaidia klabu katika kipindi hiki kigumu,'' ilimaliza taarifa hiyo.

Michezo yote Italia imesimamishwa baada ya nchi kuweka kwenye karantini hadi Aprili 3, lakini wataalamu wa afya wanasema kuzuia janga la corona kwa sasa linaweza kupita muda huo. Hivyo kuna uwezekano wa ligi Serie A kurudi upya Mei.

Wachezaji watatu wa Juventus, Daniele Rugani, Blaise Matuidi pamoja na Paulo Dybala walipatwa na virusi vya Covid-19.

Zaidi ya watu 100,000 wanaugua corona nchini Italia idadi ambayo imezidi ile ya China kulipoanza mlipuko wa ugonjwa huo mwanzoni mwa 2020.

Mapema mwezi huu familia ya Agnelli inayomiliki klabu ya Juventus ilichangia euro10 milioni katika kampeni za kupambana na corona nchini Italia.