Redondo afichua ishu ya Yondani

KIUNGO wa Biashara United, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, amefichua sababu za yeye pamoja na Kelvin Yondani wa Yanga kuendelea kuwepo katika Ligi Kuu Bara kwamba ni kutofautisha maisha yake ya ndani na nje ya uwanja.

“Nikijua nipo kazini,akili yangu inakuwa inawaza kazi, hivyo nitafanya kila kitu kinachohusiana na majukumu yangu, siwezi kuanza kuwaza kwenda kuzurura ama kufanya vitu tofauti na kitu ambacho kipo mbele yangu, sipendi kuchanganya ratiba,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Simba, Azam, Mbeya City na Ashanti United.

Alisema hilo ndilo linalowabeba pia wachezaji wenzake kama Shaban Kisiga, Kelvin Yondani, Athuman Iddy ‘Chuji’ na Haruna Moshi ‘Boban’ kwamba wanapokuwa kazini maisha yao ni tofauti na nyumbani, hivyo wanafanya kile kinachowapasa kukifanya.

“Sio soka tu bali hata shule,ukiona mwanafunzi yupo darasani akili yake inawaza kucheza disko basi ataambulia sifuri,lakini ambaye anakuwa anajua anafanya nini atafaulu masomo yake na hawezi kuona shule ni mzigo,” alisema Redondo na kuongeza; “Nimewataja hao wachezaji kwa sababu wanaweza wakakaa nje ya gemu,wakirudi viwango vyao vinakuwa pale pale ni kutokana na kujitambua kutunza vipaji vyao.”

Alisema wapo chipukizi ambao walikuwa na vipaji vya juu,lakini baadhi yao wanashindwa kutofautisha maisha ya kazi na nyumbani hivyo wanajikuta wakiporomoka na wakongwe kuendelea kucheza vizuri.

“Soka ni fursa, mimi nimeenda Ulaya kupitia kazi hiyo, hivyo lazima wajue wamechagua kazi ya maana na yenye heshima hivyo wawe wanajituma kwa bidii,” alisema.