Niyonzima atoboa siri yake na Simba

KATIKA mechi ambayo mashabiki wa Yanga walimsifu kiungo wao, Haruna Niyonzima ni ile dhidi ya Simba ambayo kiungo huyo raia wa Rwanda alikuwa amerejea Yanga.

Niyonzima aliachana na Simba na kurudi nchini kwao alikojiunga na AS Kigali, kabla ya mabosi wa Yanga kumrejesha tena nchini na kumpa mkataba.

Hata hivyo, baadhi ya mechi za awali tangu arejee Yanga baadhi ya mashabiki walimkebehi hayuko kwenye kiwango bora kama ilivyokuwa awali kabla ya kwenda Simba, usajili uliowaumiza mashabiki hao.

Kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, msimu huu, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na Niyonzima aliupiga mwingi na kufanya mashabiki waimbe jina lake.

Huku akicheka, Niyonzima anasema katika mchezo ule hakupania kama ambavyo mashabiki wengi waliamini isipokuwa alicheza akijua maumivu ya mashabiki yanavyokuwa wanapofungwa hasa na Simba.

“Sitaki kukumbuka sana mechi ile, lakini nakumbuka nilisaidiwa na mambo matatu,” anasema.

“Tuliingia uwanjani bila presha, tulijiamini na tulijua tutashinda, kocha alitupa maelekezo ya nini cha kufanya, ndiyo sababu tuliikamata Simba, tukacheza kwa kiwango bora muda wote,” alisema.

Akizungumzia mazoezi binafsi kipindi hiki cha tahadhari ya ugonjwa wa corona, alisema yana changamoto lakini kila mchezaji anapaswa kuelewa majukumu yake.

“Mazoezi binafsi na yale ya timu kuna tofauti, ukiwa na timu kuna programu ya kocha anakupangia na anakuwa anasimamia tofauti na unapojifua mwenyewe huwezi kufanya kwa asilimia 100,” alisema.

Alisema anaamini katika kikosi cha Yanga, ligi itakapoendelea watarejea kwa nguvu mpya na kuipeperusha vyema bendera ya klabu hiyo.