Ngoma aiwazia Yanga tu

KESHOKUTWA Jumamosi, Azam FC watacheza na Mbao FC wanahitaji matokeo mazuri ili kuendelea kujiimarisha nafasi bora za juu, lakini unaambiwa mshambuliaji wao Donald Ngoma anaiwaza zaidi kuifunga Yanga.

Ngoma alijiunga na Azam FC akitokea Yanga ambayo ilimsajili msimu wa 2016/17 akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, alitoa mchango mkubwa ndani ya Yanga msimu huo hadi ilipofika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na kubeba mataji mawili, Ligi Kuu na Kombe la FA.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoma alisema anatambua ana kibarua kigumu dhidi ya Mbao ambao wamefungwa mechi mbili mfululizo chini ya kocha ao mpya, Salum Mayanga.

Hata hivyo, Ngoma alisema kitu kinachomuumiza kichwa ni kukutana na timu yake ya zamani ya Yanga katika michezo yao miwili ya ligi ambayo hawajacheza.

“Tuna mchezo Jumapili na Mbao, lakini hilo halinipi shida tumejiandaa kwaajili ya ushindi na tunaweza kufanya hivyo kilichobaki kichwani kwangu kwa sasa ni michezo miwili ya ligi dhidi ya Yanga ambayo hatukucheza mzunguko wa kwanza hivyo kuwa na kiporo na mchezo mwingine wa mzunguko wa pili.

“Unajua Yanga walikuwa waajiri wangu wa zamani kila mmoja atatamani kuona nafanya nini na ninachowaambia mashabiki wangu na timu yangu watarajie mazuri.

“Unajua kabla hata kocha Hans van Pluijm hajaondoka nilikuwa naanzia benchi ni maamuzi yangu nilimuomba mwalimu anipe muda niweze kuzoea taratibu sasa niko kikosi cha kwanza na nimecheza dakika 90 dhidi ya Kagera, mambo yanazidi kuwa mazuri,” alisema.