Mwadui waikamia Simba

MWADUI FC juzi ikiwa nyumbani ilikubali kipigo kikali cha mabao 6-1 dhidi ya JKT Tanzania, lakini kocha wa timu hiyo, Khalid Adam amesema huo ndio mpira na wao wametua jijini Dar es Salaam kuwatibulia Simba.

Tangu Ligi Kuu Bara ianze mwezi Septemba, hakuna timu iliyokuwa imeshafungwa wala kufunga idadi hiyo ya mabao na Mwadui FC waliingia na rekodi ya kula kipigo kizito kabla ya raundi ya kumi kufika.

Timu hiyo inatarajia kushuka dimbani tena kesho Jumamosi kukipiga dhidi ya Wekundu wa Msimbazi, Simba - mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, huku kila upande ukihitaji ushindi ili kurejesha furaha kwa mashabiki wao.

Simba ambaye ni bingwa mtetezi atawakaribisha wapinzani hao wakikumbuka kupoteza mechi mbili mfululizo - matokeo ambayo yamewafanya mashabiki kukunja uso, hivyo kufanya mechi hiyo kuwa na ushindani mkali.

Adam aliliambia Mwanaspoti kuwa licha ya maumivu waliyopata juu ya matokeo hayo, lakini huo ndio mpira na timu yoyote hufungwa, hivyo wanakwenda kujiuliza kwa Simba.

“Tunajua wote tumepoteza mchezo uliopita, kwa hiyo tunaenda kupambana kila mmoja kusaka pointi tatu, hatuwezi kuwaogopa tunachotaka ni kuona haturudii makosa yale, vijana wako fiti nilioondoka nao,” alisema kocha huyo.

Hata hivyo, Adam aliongeza kuwa siyo mara ya kwanza kukutana na timu hiyo na kila mmoja alishapata matokeo ya aina yoyote, hivyo mbinu na nidhamu ya mpira ndiyo itawapa faida ugenini, lakini lengo ni kuhakikisha kuwa wanaondoka na alama tatu.