Mtego wa Yanga, Azam Ligi Kuu kumbe uko hapa

KUMBE wanachofanya Namungo ni sawa na kumkimbiza mwizi kimya kimya. Kocha wa Namungo, Hitimana Thierry amesema kama wachezaji watacheza kwa jihadi na nidhamu katika michezo iliyosalia basi wanaweza kumaliza nafasi ya pili katika Ligi.

Ligi Kuu Bara ambayo ilisitishwa miezi miwili iliyopita kutokana na janga la virusi vya corona, inatarajiwa kurejea Juni mosi baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli kuruhusu shughuli mbalimbali za kimichezo kuendelea nchini.

Hitimana ambaye kwa sasa yupo kwao ambako kuna marufuku ya mtu yeyote kutoka wala kuingia nchini humo kutokana na janga la virusi vya corona, alisema inawezekana kuzishusha Azam na Yanga ambao wapo katika nafasi ya pili na tatu katika msimamo wa Ligi.

Mrwanda huyo, alisema pamoja na uchanga wa timu yake na uzoefu mdogo wa wachezaji wake, wanaweza kumaliza nafasi hiyo, “Nani alijua kama Leicester City wanaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England siku moja tena mbele ya Chelsea, Manchester United, Liverpool, Arsenal na Manchester City?

“Nina imani kubwa na wachezaji wangu kuwa tunaweza kufanya jambo katika mchezo iliyosalia ya Ligi. Mapumziko ya corona yamewapa muda mzuri wa kutuliza miili yao na akili hivyo tutaendelea na Ligi kama tunaanza msimu mpya vile,” alisema.

Simba wana pointi 71, Azam ambao wapo nafasi ya pili wana pointi 54, Yanga wenye mchezo mmoja nyuma wana pointi 51, vijana wa Hitimana wamevuna pointi 50 katika michezo 28 sawa na Azam na Simba.

Kocha huyo wa zamani wa Biashara United aliendelea kuliongelea hilo kwa kusema, “Utofauti na pointi sio mkubwa baina yetu hivyo tunawajibika kwa kila mchezo ambao utakuwa mbele yetu tucheze kama fainali.”

Kwa sasa Namungo ambao wameanza mazoezi ya pamoja wapo chini ya kocha msaidizi Godfrey Hokoko ambaye amekuwa na mawasiliano ya karibu na Hitimana.