Morrison aishtaki Yanga TFF, Simba nayo yashtakiwa

Dar es Salaam. Kiungo mshambuliaji wa timu ya Yanga, Bernard Morrison amefungua kesi dhidi ya klabu hiyo akidai kutotambua mkataba mpya unaodaiwa kuwa alisaini wa miaka miwili.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa jana na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya mwenyekiti wake, Elias Mwanjala.

Mwanjala alisema mchezaji huyo amewasilisha ushahidi wake katika kesi hiyo ambayo uamuzi unaweza kutolewa leo kutegemeana na usikilizaji wa pande zote, mashahidi na kamati kuridhishwa na ushahidi utakaowasillishwa.

Alisema Morrison ambaye aliifungia Yanga bao katika ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, amefungua kesi hiyo mwenyewe na alifika kwa ajili ya utetezi wa hoja zake huku Yanga ikiwakilishwa na viongozi mbalimbali akiwemo mwanasheria ambaye pia ni kaimu katibu mkuu, Simon Patrick na makamu mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela.

“Sisi kazi yetu ni kusikiliza na kupitia ushahidi ambao pande zote mbili umewasilisha kwetu. Kama hautoshi, basi tutawapa muda zaidi, lakini kama tumeridhishwa tutatoa uamuzi, lakini siyo leo (jana) kwani kuna malalamiko mengi ukiachana na hayo,” alisema Mwanjala.

Alisema kuwa mbali ya kesi hiyo, kamati yake pia inasililiza malalamiko yaliyowasilishwa na Yanga dhidi ya Simba ikiituhumu kufanya mazungumzo na Morrison kinyume na utaratibu, ikidai amekuwa akishawishiwa na mabingwa hao ajiunge nao.