Messi aweka tiki usajili wa Lautaro Martinez

Thursday May 21 2020

 

BARCELONA, HISPANIA. MMESIKIA huko? Supastaa, Lionel Messi anaripotiwa kuweka tiki kwenye mpango wa Barcelona wa kumsajili mshambuliaji wa Kiargentina, Lautaro Martinez kwenye dirisha lijalo.

Kwa muda mrefu miamba hiyo ya La Liga imekuwa ikitajwa kuwa na mpango wa kumsajili straika huyo wa Inter Milan na Messi sasa ameibuka na kumzungumzia mchezaji huyo, akisema “Ni mshambuliaji aliyekamilika.”

Barca wanafukuzia huduma ya Martinez ili kwenda kurithi mikoba ya straika Luis Suarez, ambaye tayari umri umeshaanza kumtupa mkono.

Martinez ndio kwanza ana umri wa miaka 22, hivyo anatazamwa kama mrithi wa muda mrefu wa Suarez, ambaye alikosa mechi kibao za msimu huu kwenye La Liga kutokana na kuwa majeruhi.

Hata hivyo, Inter Milan wameendelea kung’ang’ania bei iliyobainishwa kwenye mkataba wake kwamba timu inayotaka kumnunua basi itapaswa kulipa Pauni 98.9 milioni, jambo ambalo linadaiwa linaweza kuwa kikwazo kwenye kukamilika kwa dili hilo.

Lakini, kauli ya Messi inaweza kuweka uzito na mabosi wa Barcelona wakaamua kufanya kweli kunasa saini yake.

Advertisement

“Nadhani ni mshambuliaji aliyekamilika. Ana nguvu na anaweza kukokota mipira na jicho la kuona goli, anafahamu pia namna ya kulinda mpira,” alisema Messi.

“Lakini, tunasubiri kuona nini kitatokea kwa upande wake na wachezaji wengine wanaotajwa.”

Martinez, ambaye alicheza na Messi kwenye timu ya taifa ya Argentina, amefunga mabao 16 na kuasisti manne katika mechi 31 alizocheza za michuano yote akiwa na kikosi cha Inter Milan msimu huu.

Advertisement