Mechi 15 za ubingwa Yanga

YANGA imeweka wazi malengo ya kutafuta taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara wakitaka katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza wasiwe wamepoteza wala kutoka sare mechi nyingine.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hersi Said alisema wanataka kuhakikisha mzunguko wa kwanza mpaka unakamilika timu yao iwe katika ubora wa kutopata matokeo ya kuwapunguzia pointi. “Tulipoanza ligi tukatoa sare na Prisons, wapo ambao walidhani ni udhaifu wa timu yetu, lakini wao walipokutana na timu hiyo wakapoteza, pia tulikutana na Mtibwa Sugar tukashinda kwa bao 1-0 tukaonekana kama timu yetu dhaifu, lakini washindani wetu wakubwa wapo waliopoteza na wengine kutoa sare katika uwanja huohuo,” alisema.

Hersi ambaye alihusika kwa asilimia zote katika usajili wa timu hiyo msimu huu alisema: “Yanga tathimini yetu tunaona tuna ligi ngumu msimu huu kila timu imejiandaa vyema kiushindani, lakini pia tunaona tuna kikosi imara ambacho tunatakiwa kukiamini na kuendelea kukijenga.”

“Hatua kubwa tunayotaka kuhakikisha sasa tunaisimamia ni kuendelea kushinda mechi zetu, naona ndani ya mechi 15 au nusu msimu tutakuwa na timu bora ambayo itatupa uhakika wa ubingwa msimu huu, tunataka kuendelea kushinda lakini pia kama tutapata sare zisiwe kwa idadi kubwa,” alisema Hersi ambaye yupo na timu hiyo Kanda ya Ziwa.

Bosi huyo ambaye pia ni mkurugenzi wa uwekezaji wa GSM ambao ni miongoni mwa wadhamini wa Yanga, alisema kikosi chao kucheza bila kupoteza inathibitisha uimara wa ukuta wakijitofautisha na timu zingine.

“Hatujafungwa mpaka sasa, hii maana yake tuna safu nzuri ya ulinzi ambayo tunatakiwa kuendelea kuijenga zaidi, pia hakuna mechi ambayo tumemaliza mpaka sasa bila kupata bao, kiu yetu ni kuona tunatanua zaidi ushindi wetu kwa kupata mabao mengi na hili litakamilika baada ya muunganiko mzuri kupatikana.

“Tuna changamoto ambazo ni benchi jipya linatakiwa kutafuta utulivu na uimara katika kutoa mbinu zake.”