Mbunge Chadema ‘ataja sababu’ kipigo cha Taifa Stars

Monday June 24 2019

 

By Mwandishi Wetu

Dodoma. Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga amesema huenda wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kulipwa posho kiduchu kumechangia kufungwa mabao 2-0 na Senegal katika mchezo wao kwanza katika Fainali za Mataifa ya Afrika (CHAN) zinazoendelea nchini Misri.

Haonga ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 24, 2019 bungeni jijini Dodoma baada ya kuomba mwongozo, akibainisha kuwa kuna tetesi kuwa badala ya Serikali kuwalipa wachezaji hao Dola 300 za Marekani, wamelipwa Dola 70.

“Habari zilizopo ni kuwa wamelipwa Dola 70 badala ya Dola 300. Tunaamini unapoingia katika michezo lazima uwe na hali nzuri ya kupambana.”

“Kuna taarifa kwamba kuna siku moja wachezaji hawa hawakufanya mazoezi na kufanya mgomo wa kimya kimya. Kwanini Serikali haiwapatii posho wachezaji hao kwa sababu michezo hiyo (Afcon) inaendelea hivi sasa. Tuongoze katika hili kwanini Serikali isiwapatie fedha,” amesema Haonga.

Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia amesema hawezi kujibu kwa kuwa si jambo lililotokea bungeni leo kulingana na kanuni za Bunge zinavyoelekeza.

Advertisement