Mafundi, wape Friikiki wakumalize

SIO kila mtu anaweza. Inahitaji utaalamu, mazoezi ya kutosha na utulivu wa hali ya juu. Kufunga mabao ya friikiki, sio rahisi kama unavyofikiria. Inaitwa weka mbali na watoto. Ni zaidi ya sayansi. Ni zaidi ya kupiga tu. ni uchawi! Ni kitu gani, kinachofurahisha zaidi kwenye soka. Kinachoburudisha macho na moyo? Mchezaji kupita katikati ya msitu wa mabeki?

Upigaji wa penalti kwa staili ya ‘panenka’ au mabao ya kubetua kama anavyopenda kufanya Lionel Messi? Acha nikuibie siri, hakuna kinachoburudisha nafsi ya shabiki wa soka, kama kushuhudia friikiki tamu, inayoelea moja kwa moja hadi kwenye nyavu za timu pinzani. Walikuwepo mafundi wa kazi hiyo, Beckham, Juninho, Roberto Carlos na Ronaldinho, walitisha sana. Hicho ni kizazi cha jana na juzi. Lakini hata katika kizazi hichi cha sasa, wapo mafundi.

Tena mafundi kweliweli. Ukianza kuwahesabu wala hutowamaliza, maana kizazi bado kingalipo. Hawa hapa ni wapiga friikiki watano, hatari zaidi duniani ambao bado wanacheza soka:

5. Aleksandar Kolarov

– mabao 22

Ni mabeki wachache sana, wanaoweza kufikia hata nusu ya uwezo wa Aleksandr Kolarov. Ni mmoja wa mabeki fundi wa kutupia kambani. Kolarov (34), amefunga asilimia 35 ya mabao yake, kwa njia ya friikiki. Haijawahi kutokea kwa mabeki!

Nyota huyu wa zamani wa Man City na AS Roma, mara nyingi hujulikana kama ‘Roberto Carlos’ wa Serbia, kutokana na uwezo wake mkubwa kufunga mipira iliyokufa.

Upigaji wake, kwa kiasi kikubwa, kinashabihiana na lejendari huyo wa Brazil. Kinachombeba Kolarov, ni uwezo wa kufunga friikiki, hata kwa kutumia upenyo mdogo sana, na umbali mfupi kutoka eneo la lango la timu pinzani. Unakumbuka alichowafanya Costa Rica (2018 World Cup), na lile aliloifungia AS Roma, dhidi ya Athletic Bilbao (2019)?

4. Hakan Calhanoglu

– mabao 26

Kama ni mfuatiliaji mzuri wa Bundesliga, basi utakuwa umeshuhudia uwezo wa Hakan Calhanoglu, wa kupiga mipira iliyokufa, sanasana mashuti ya moja kwa moja. Anapopata fursa ya kupiga friikiki, nyavu za timu pinzani, hutoa majibu.

Hivyo ndivyo, kiungo huyo wa zamani wa Hamburger SV, alivyo mkali. Takwimu inaonesha kuwa, asilimia 38 ya mabao ya mturuki huyo, ikiwemo alizofunga akiwa Karlsruher SC, zimetokana na friikiki.

Nani anaweza kusahau, uwezo mkubwa aliouonesha katika msimu wa 2014-15, alipoifungia Bayer Leverkusen, mabao tisa ya friikiki? Ndio, yote hayo katika msimu mmoja. Chukua hiyo!

Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana, Umahiri wa Calhanoglu, wa kupiga friikiki, umeshuka sana tangu ajiunge na AC Milan, mwaka 2017, ambapo rekodi inaonesha, amefunga mabao matatu tu ya friikiki.

3. Miralem Pjanic

– mabao 26

Miralem Pjanic, alifunga mabao ya hatari sana ya friikiki, akiwa pale Serie A. Licha ya kuifikia rekodi ya Calhanoglu, Mbosnia huyu, yuko juu ya Hakan, kwenye orodha hii, kutokana na idadi kubwa aliyofunga katika miaka ya hivi karibuni.

Katika kikosi cha Juventus, alikabidhiwa jukumu hilo, sambamba na Cristiano Ronaldo na Paolo Dybala, lakini amini usiamini, Pjanic amewafunika Ronaldo na Dybala, kwa idadi kubwa ya mabao ya friikiki alizofunga, ndani ya jezi ya Bianconeri.

Pjanic (30), ambaye kwa sasa anakipiga pale Camp Nou, bila shaka atakuwa ndio mpigaji wa friikiki namba mbili, baada ya Lionel Messi, ambaye ni chaguo la kwanza, lakini kutokana na umahiri wake mkubwa, Blaugrana watalazimika kumuweka moyoni!

Kiungo huyo wa Bosnia, amefunga mabao 22, katika maisha yake ya kucheza soka la klabu, na mengine manne, kwa timu yake ya taifa. Halafu usichokijua ni kwamba, asilimia 68 ya mabao hayo ya friikiki, amefunga katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni.

2. Lionel Messi

– mabao 53

Lionel Messi, amefunga mabao 21 ya friikiki, kwa klabu na taifa lake la Argentina, ndani ya misimu mitatu ya hivi karibuni pekee. Nikushangaze kidogo? Ni hivi, Lionel Messi, hakuwa mpigaji wa friikiki, lakini alikuja kujifunza na hivi sasa, ni moto wa kuotea mbali.

Muargentina huyu, anayeaminika kuwa mmoja wa ‘miungu wa soka’, amekuwa vizuri katika miaka ya hivi karibuni. Unakumbuka goli la yadi 35, alilowafunga Liverpool, mwaka jana?

Au Shuti alilofumua mwaka 2016, katika mchezo kati ya Argentina na Marekani? Mwaka 2012, alifanya hivyo dhidi ya Real Madrid, unakumbuka?

Katika mabao yake 53 za friikiki, Messi amefunga 47 akiwa na jezi ya Barca, huku zilizobaki sita, akiifungia Argentina. Friikiki kwa Messi, ni sawa na mkwaju wa penalti. Akipata nafasi moja hakuachi!

1. Cristiano

Ronaldo

– mabao 57

Cristiano Ronaldo, atabaki kuwa Cristiano Ronaldo. Huyu ni zaidi ya mnyama. Kila mahali yupo. Anakupatia kila kitu unachotaka. Katika ufungaji nako, atakupatia zaidi ya burudani.

Anafunga kwa kichwa, mguu wa kulia, wa kushoto, yaani kila kiungo! Lakini ukiachana na uwezo wake mkubwa dimbani. Ukiachilia mbali mjadala wa nani mkali kati yake na Lionel Messi, chuki mchukie, lakini Mreno huyo ni habari nyingine katika upigaji wa friikiki.

Katika kizazi cha sasa, hakuna kama CR7! Ni kweli, kadri anavyozidi kuzeeka, ndivyo uwezo wake wa kupiga friikiki unavyopungua, lakini ukweli utabaki kuwa, Ronaldo ni mmoja wa viumbe hatari wa kupiga friikiki, wanaoishi kwenye ulimwengu wa soka. Mpaka kufikia sasa, ameshatupia mara 57.

BABA LAO

Wakati takwimu hizo hapo juu za wanasoka ambao bado wanasakata kabumbu zikionyesha, Ronaldo hana mpinzani, takwimu za wapiga friikiki bora wa zama zote zinaonyesha kuwa, gwiji wa Brazili, Juninho Penambucano ndio baba lao.

Juninho, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 45, alikuwa habari nyingine, katika upigaji wa friikiki. Mkali huyo wa zamani wa Olympique Lyon, Vasco da Gama, Al-Gharafa na klabu yake ya nyumbani ya Sport Club do Recife, alifunga mabao 77 ya friikiki.

Haikujalisha amesimamia wapi, kushoto, kulia au hata katikati mwa uwanja, Juninho angemtungua kipa yeyote yule, kwa urahisi. Kwa mujibu wa Juninho, alijifunza kupiga friikiki kwa kumuiga Mbrazili mwenzake, Marcelinho, aliyefunga mabao 59 ya friikiki.

“Nilianza kwa kumuiga nyota wa zamani wa Corinthians, Marcelinho. Alikuwa fundi hasa wa friikiki. Huyu ni mchezaji wa kwanza niliyemshuhudia akipiga mpira, ukaelea hewani. Alikuwa hatari sana,” Juninho alisema, alipoulizwa kuhusu uwezo wake wa kupiga friikiki.

“Hiyo inatosha kuonesha kuwa, tekniki hii sio yangu, hata Didi, aliyeshinda Kombe la Dunia, mwaka 1958 na 1962, pia alikuwa mkali wa kupiga friikiki. Kila mtu anaweza kufanya hivyo, akiamua kujifunza na kutulia,” aliongeza.

Gwiji wa Brazil, na mmoja wa wafalme wa Soka, Pele, ni wa pili katika orodha ya wakali wa muda wote wa kufunga friikiki. Pele, alitupia kambani mara 70. Mshindi wa Ballon d’Or wa mwaka 2005, Mbrazili Ronaldinho anashika nafasi ya nne, akiwa na mabao 66.

Muingereza David Beckham, mkali wa kukunjuka, anashika nafasi ya tano, akiwa amefunga mabao 65 ya friikiki. Zico na Diego Maradona, walifunga mabao 62 kila mmoja. Beki pekee katika 10 bora ni kocha wa sasa wa Barcelona, Mholanzi Ronald Koeman, alifunga mabao 60.

Aidha, anayekamilisha 10 bora ya wakali wa kufunga mabao ya friikiki, ambayo imetawaliwa na wanasoka wa Brazili, sio mwengine bali ni golikipa Rogerio Ceni, ambaye katika maisha yake ya kucheza soka, alifunga friikiki 59.