Madhara ya barakoa kwa wachezaji

KWA sasa kila kona Watanzania wanatembea wakiwa wamevaa barakoa kwa ajili ya kujikinga na virusi vya corona na juzi nyota wa Yanga, Bernard Morrison ‘BM33’ alionekana akipiga tizi na wenzake akiwa amevaa barakoa na kushtua baadhi ya mashabiki.

Hata hivyo, madaktari wametoa tahadhari juu ya utumiaji wa barakoa kwa wachezaji kipindi wanapokuwa wakifanya mazoezi, kwa nia ya kujiweka salama kwani kifaa hicho sio salama kwa wanaofanya kazi ngumu kama mazoezi hasa ya soka.

Licha ya Daktari wa Yanga, Shecky Mngazija kufafanua kuwa, matumizi ya barakoa hayana shida kama maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya yatafuata inavyotakiwa.

“Kifupi barakoa haizuii upumuaji labda kwa mtu ambaye ana matatizo katika mfumo wake wa upumuaji, lakini kama huna tatizo unaweza ukafanya mazoezi huku umeivaa,” alisema Dk Mngazija aliyedai barakoa aliyovaa Morrison ni zile zinazoruhusiwa.

“Lakini, kama una tatizo hata kama unatembea ukiwa umeivaa inakuwa shida, kitu cha msingi wachezaji na watu wote wanapaswa kuchukua tahadhari muda wote,” alisema Dk Mngazija.

Aliongeza kwa mchezaji anayefanya mazoezi, huku amevaa barakoa na akagundua inamletea shida au inambana ni vyema akaomba ushauri kwa wataalamu wa afya ili aweze kusaidiwa.

“Kitu chochote kinachokuletea shida lazima ukiache, hata dawa ukiona inakuvimbisha au inakuwasha unashauriwa kuiacha.

Naye Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema kitaalamu mchezaji anapofanya mazoezi anatakiwa kupata hewa ya kutosha kwa sababu uhitaji wa hewa unakuwa mkubwa.

“Kuna barakoa ambazo ni ‘spesho’ kwa mazoezi, lakini kama anavaa ile ya kawaida, uhitaji wake wa oksijeni unakuwa hautoshi na matokeo yake hataweza kufanya mazoezi vizuri.

Moja ya athari ambazo mchezaji anaweza akapata kwa kuvaa barakoa ambazo sio za mazoezi ni pamoja na kukosa nguvu na kufanya mapafu kuleta shida,” alisema Dk Gembe.

Kwa upande wa Daktari Shita Samweli, ambye pia ni mchambuzi wa safu ya Daktari wa Mwanaspoti, alisema kitaalamu barakoa ina vitundu ambavyo vinapitisha hewa, lakini huwa inazuia kuingia kwa hewa ya kutosha.

“Kuna utofauti wa kupumulia hewa ya kawaida na kupumua ndani ya barakoa, lakini kazi ya barakoa ni kuzuia mate kutoka kwa mtu mwenye maambukizi,” alisema Dk Shita na kuongeza;

“Mchezaji anapocheza anavuta hewa kwa haraka na kuitoa kwa lengo la hewa kwenda kwa haraka kwenye misuli, kwani uhitaji wa hewa kwa anayefanya mazoezi inakuwa kubwa kuliko aliyekaa, hivyo anapovaa barakoa lazima kuwe na ugumu fulani.”

Aliongeza anapoonekana mchezaji amevaa barakoa, basi hayupo vizuri kwa afya na ameshauriwa kufanya hivyo ili kuwalinda wenzake.

Sebastian Mapunda, Daktari wa KMC alisema mchezaji anapovaa barakoa huku akifanya mazoezi kunakuwa na ugumu wake.

“Mtu yeyote anapofanya mazoezi anatakiwa kupata hewa ya ziada ili kuruhusu misuli kufanya kazi yake vizuri, sasa kitendo cha kuvaa barakoa anaweza kusababisha upungufu wa oksijeni.

“Anayevaa barakoa huku anafanya mazoezi atapata shida kwenye kupumua na mwisho wa siku ataleta shida kwenye mfumo wake wa upumua, kwani awali barakoa ilikuwa inavaliwa na wataalamu wa afya kwa sababu maalumu lakini kutokana na tatizo hili ndio maana kila mtu sasa anavaa,” alisema Mapunda.

YANGA WAPEWA MASHARTI

Dk Mngazija alisema katika kuzingatia hayo, wachezaji wa Yanga wamepewa elimu kuzingatia vitu 12 ili kupambana na corona.

“Kitu cha kwanza ni kuvaa barakoa muda wote akiwa mazoezini na kambini, kunawa mikono kwa maji tiririka, kuvaa ‘gloves’, kutumia vitakasa mikono, unapohisi dalili yoyote inampasa kuwahi hospitali na kuepuka mikusanyiko.

“Kuepuka kujishika pua, mdomo na macho, mchezaji anapokohao ahakikishe anaziba mdomo kwa kitambaa au kutumia kiwiko cha mkono, kukaa umbali kuanzia mita moja, kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono, kuepuka kukumbatiana, na kuepuka kuvua viatu ndani,” alisema.