MWASHIUYA: Burungutu Yanga lilinichanganya

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Geofrey Mwashiuya, anasema burungutu la noti alilowekewa mezani wakati ule lilimvuruga akaona nyota akasaini fasta bila kujijua.

Mwashiuya alitua Yanga 2015 akitokea kwao Mbozi katika timu ya Kimondo iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza kwa kandarasi ya miaka mitatu.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mwashiuya alisema: “Nilipoona ile pesa mezani nilikuwa kama chizi kwani sikuwahi kuona pesa nyingi hivyo kuzimiliki mimi zaidi ya laki moja hivyo kuona milioni 2 nilichanganyikiwa japokuwa nilimpigia kwanza simu kaka yangu kumwambia akaniambia nichukue tu.”

Mwashiuya alisema, hata alivyoambiwa mshahara Sh400,000 hakuona shida kwa kuwa zilikuwa pesa nyingi kuwahi kuzimiliki tangu azaliwe.

Alisema baba ake mdogo ndiye alikuwa kama mlezi wake baada ya baba ake mzazi kufariki akiwa mdogo, ila wakati anaitwa na Yanga mzazi wake huyo hakuwepo nchini alikuwa Zambia katika kazi zake za Udereva wa malori.

“Baada ya Baba mdogo kurejea nikamweleza aliwaka sana akasema pesa hizo ni ndogo sana na ndipo Yanga wakaniongezea Mil 10 baada ya Baba kuwa mkali ikawa jumla Mil 12 na mshahara wakaniongezea mpaka 800,000 ndipo nikawa nimeongezewa mwaka wa tatu kwa gharama hiyo.”

Mwashiuya alisema, pesa zote hizo kwake zilikuwa nyingi sana aliamua kuzipeleka kwa mama yake mzazi huko Mbozi zikamsaidia kujenga nyumba nzuri ambayo anaishi hadi sasa.

Yanga walimwona Mwashiuya ambaye kwa sasa anakipiga Kagera Sugar, katika mchezo wa Ligi Daraja la kwanza uwanja wa Karume wakati timu yake ya Kimbondo ilipokuwa ikicheza na Friend Rangers na ndipo wakachukua namba zake za simu na kuanza mawasiliano naye.