Lionel Messi adaiwa kupanga kuitema Barcelona mwakani

Barcelona, Hispania. Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi yuko tayari kuachana na timu hiyo mkataba wake utakapofikia mwisho mwishoni mwa msimu ujao, imeripotiwa.

Messi amesitisha mazungumzo ya mkataba mpya baada ya kukasirishwa na ripoti kwenye vyombo vya habari vinavyomtuhumu alihusika kwa kiasi kikubwa kufukuzwa kazi kwa kocha Ernesto Valverde, Januari, mwaka huu.

Hiyo ni kwa mujibu wa kituo cha redio cha Hispania, Cadena Ser, ambapo imeripotiwa pia staa huyo wa Kiargentina hafurahishwi na ubora wa viwango kwenye kikosi hicho kwa sasa na hivyo anafikiria kuondoka mwishoni mwa msimu ujao.

Jambo hilo linaibua uvumi mkubwa wa wapi Messi anaweza kwenda msimu ujao, huku sehemu kadhaa zikitajwa ikiwamo kuungana na kocha wake wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola huko Manchester City.

Mkataba wa Guardiola huko Manchester City utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao na bado haijafahamika kama atasaini kuendelea kubaki kwenye kikosi cha miamba hiyo ya Ligi Kuu England.

Messi alitesa chini ya Guardiola alipokuwa Barcelona kati ya mwaka 2008 na 2012, ambapo wawili hao walishinda La Liga mara tatu, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili na Klabu Bingwa Dunia mara mbili.

Ripoti ya Cadena Ser inadai Messi na baba yake, Jorge walianzisha mazungumzo ya kusaini mkataba baada ya ule wa sasa uliosainiwa 2017 kuelekea mwishoni, lakini mambo yamebadilika na hataki kubaki Camp Nou. Messi, alitimiza miaka 33, mwezi Juni.