Kwa hawa... Simba Yanga Watazidunda

USAJILI haujaanza rasmi lakini vyanzo sahihi vimeithibitishia Mwanaspoti kwamba, Simba na Yanga zina mchuano mkali kwa wachezaji wanne lakini bei ya straika Mburkina Fasso, Yacouba Sogne imewashtua.

Habari zinasema kwamba mchezaji huyo amewaambia kwa nyakati tofauti kuwa, anataka Sh230 milioni na hatakaa kwenye klabu hizo zaidi ya miaka miwili. Kisha Yacouba mwenyewe amesisitiza kwamba; “Corona ikiisha nitatoa msimamo rasmi.”

Na kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay amesisitiza kwamba kazi ipo tena pevu.

Habari za uhakika zimethibitisha kwamba, timu hizo mpaka sasa kuna wachezaji ambao Kocha wa Yanga, Luc Eymael amesisitiza ni lazima nguvu ya fedha itumike kuwapata huku Ofisa Mtendaji wa Simba, Senzo Mazingisa akikiri kuwa wakati wa usajili huwa na mambo mengi hasa kwa klabu kubwa kama yao.

Katika idadi hiyo ambayo wengine wao wamethibitisha kuzungumza na klabu zote mbili, wapo mastraika watatu hatari huku mmoja tu akiwa beki na mzawa ambaye kila siku mpya ikianza amekuwa akipanda thamani.

Sogne Yakouba (Burkina Fasso)

Ni straika aliyemaliza mkataba na Asante Kotoko ya Ghana msimu huu na amegoma kuongeza akarudi kwao. Klabu kadhaa zinamtaka za Ghana lakini anataka zaidi ya Sh230milioni ndio maana zimemkaushia.

Simba walianza naye, kisha Yanga wakaingilia hivi karibuni lakini bado amekomaa na hakuna aliyeweza kufikia muafaka kutokana na Sh230milioni ambazo vigogo hao wanaamini hana thamani hiyo. Mtandao wa Ujerumani wa transfermarkt unasema thamani yake haitazidi Sh180milioni.

Michael Sarpong (Ghana)

Huyu ni straika Mghana ambaye Rayon imemvunjia mkataba kwa madai kwamba amemjibu vibaya Rais wa klabu hiyo baada ya kuambiwa mshahara wake utakatwa wakati huu wa corona.

Yanga ndio waliotajwa kutangulia kumshawishi mshambuliaji huyu ambaye mwenyewe ameifichulia Mwanaspoti kuwa amepigiwa na mtu wa Simba naye akampa mahitaji yake hivyo ni suala la muda tu na atakayemrudia vizuri na kwa wakati.

“Safari hii baada ya mimi kuvunja mkataba na Rayon, Yanga wakarudi tena na ofa yao ilikuwa nzuri kidogo ingawa sasa Simba nao wamekuja nao wanataka kunisajili sasa sijajua ni wapi nitacheza katika timu hizo mbili, muhimu nitaangalia wapi watanipa ninachotaka na sehemu ambayo nitakuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.” Habari za ndani zinasema kwamba baadhi ya vigogo wa Simba wanahofia nidhamu yake.

Mpiana Mozizi (DR Congo)

Straika wa FC Lupopo ambaye ni mmoja kati ya wafungaji bora watatu wa msimu huu pale DR Congo ambaye naye amezigonganisha klabu mbili za Kariakoo.

Ubora wake wa kufunga umemwezesha kushinda tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya DRC msimu huu uliovunjwq kabla ya kumalizika na TP Mazembe kutangazwa mabingwa kutokana na janga la corona. Amefunga mabao 12 sawa na Jackson Muleka wa TP Mazembe na Fiston Mayala wa AS Vitta amefichua kwamba Simba ndio walitangulia kumfuata ingawa sasa wakati wowote atasaini Yanga.

“Nilikuwa na mazungumzo na bosi mmoja wa Simba kwa muda mrefu, alikuwa anakuja sana hapa Congo hasa Lubumbashi akaniambia mambo mengi lakini Yanga nao wakaja hapa karibuni na mambo yao yalikuwa makubwa kidogo nafikiri huenda nikacheza Yanga, “ alisema Mozizi.

Bakari Mwamnyeto (Coastal Union)

Beki huyo mzawa ambaye naye amezipigisha shoti klabu mbili kongwe na vita hiyo bado inaendelea kibabe ingawa amekiri Yanga wamempelekea mkataba wa awali asaini akawaambia watulie kidogo hadi wakala wake, Kassa Musa arejee kutoka Italia.

Yanga ndio waliotangulia kumfuata beki huyo na Mwanaspoti linafahamu kazi hiyo ilifanywa na Mwenyekiti wao Dk Mshindo Msolla baadaye Simba wakaingilia na hata wiki iliyopita wakala wake alikiri Simba wamemwambia asisaini Yanga kuna ofa mpya wanapeleka.

Ally Mayay ambaye ni mchambuzi wa soka ameiambia Mwanaspoti kuwa; “Naona hawana watu bora na makini katika kusaka vipaji hili ambalo linaendelea, unajua kila klabu ina mahitaji yake na naamini yanatofautiana.”

“Kugongana kwa wachezaji wa aina moja huo ndio udhaifu wa hao wanaowatafutia wachezaji wapya.

Hilo pia linaweza kusababishwa na utani wa jadi, klabu moja kati ya hizo inaweza kuona mwenzake anamtaka fulani wakasema hapana wale wakimpata yule watatuumiza ngoja tukawapokonye, hili linaweza kuwa na athari lakini mara nyingi anayekwenda kuathirika sana ni mchezaji kama anakuwa amefanya uamuzi bila kuangalia aendako.”