Nyota Tanzania Prisons wapata ahueni

Muktasari:
- Kipa wa timu hiyo, Mussa Mbisa amesema walikuwa wanaishi kwa presha kubwa na kuumiza vichwa namna ya kuhakikisha timu inasalia salama, licha ya kutokuwa nafasi nzuri ila anaona wamepata ahueni ya kubakia Ligi Kuu.
TANZANIA Prisons kukaa nafasi ya 11 katika Msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imecheza mechi 28, imeshinda nane, sare sita, imefungwa 14 na kukusanya pointi 30 ni kicheko kwa wachezaji wa timu hiyo wakiamini kwamba wamepata ahueni.
Kipa wa timu hiyo, Mussa Mbisa amesema walikuwa wanaishi kwa presha kubwa na kuumiza vichwa namna ya kuhakikisha timu inasalia salama, licha ya kutokuwa nafasi nzuri ila anaona wamepata ahueni ya kubakia Ligi Kuu.
Mbisa amecheza mechi 22, akiwa na cleansheet tano na kuruhusu mabao 23 amesema: "Msimu huu ulikuwa mchungu sana kwetu, lakini hatukuwahi kukata tamaa kupambana, angalau nafasi tuliyopo tunaona mwanga wa kusalia Ligi Kuu.
"Ili tuwe na uhakika zaidi tunatakiwa kushinda mechi ngumu mbili zilizosalia mbele yetu dhidi ya Yanga na Singida Black Stars ambayo tutaifuata kwao."
Mchezaji mwingine aliyefurahishwa na timu hiyo kushika nafasi ya 11 ni mshambuliaji Jeremiah Juma aliyesema:" Jambo kubwa kwetu ilikuwa ni timu kusalia Ligi Kuu, hilo tunaliona linakwenda kutimia, kikubwa ni kupambana na mechi zilizosalia."
Kwa upande wa meneja wa timu hiyo, Benjamin Asukile amesema: "Mbele yetu tuna mechi mbili ngumu, ila naamini kwa sasa wachezaji wana morali ya juu wanaweza wakashinda michezo hiyo."