Kiungo Kenny Ally aitosa Yanga kutua KMC

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa kanuni za usajili, mchezaji akibakiza mkataba wa miezi sita anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine ikiwemo kupewa mkataba wa awali jambo ambalo tayari limefanyika kati ya KMC na meneja wa mchezaji huyo, Maka Mwalwisi.

Dar es Salaam.Yanga wamegonga mwamba kuinasa saini ya kiungo Kenny Ally yuko mbioni kujiunga na KMC kwa mkataba wa miaka miwili Juni 30.

Yanga ilikuwa inasubiri saini ya mchezaji huyo ambaye anamaliza mkataba na Singida United iliyo chini ya Mkurugenzi wao Mwigulu Nchemba.

Singida United ilimsajili Kenny akitokea Mbeya City kwa mkataba wa miaka miwili ambapo imeelezwa kwamba hata huko KMC amepewa mkataba wa miaka miwili.

Kwa mujibu wa kanuni za usajili, mchezaji akibakiza mkataba wa miezi sita anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine ikiwemo kupewa mkataba wa awali jambo ambalo tayari limefanyika kati ya KMC na meneja wa mchezaji huyo, Maka Mwalwisi.

Mwalwisi alifikia uamuzi ya kufanya mazungumzo na KMC baada ya ukimya uliokuwepo dhidi ya uongozi wa Singida United na hata alipowaandikia barua ya kukumbushia mkataba wa mchezaji wake, walimruhusu kuendelea na mazungumzo na timu nyingine, kwa ufupi walimtakia kila lenye kheri mchezaji huyo.

Imeelezwa kwamba mchezaji huyo bado anaidai pesa ya mishahara Singida United kiasi cha Sh14 milioni na kwamba kiasi hicho kisingekuwa tatizo ya kufanya mazungumzo mengine na timu hiyo ya kuongeza mkataba ama kwenda timu yoyote ikiwemo Yanga endapo wangeonyesha nia ya kumhitaji.

"Tumefanya mazungumzo na KMC na kwa asilimia 95 tumefikia pazuri, tunasubiri ifike Juni 30 ili tumalize kila kitu, Yanga hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanywa na sisi, nilijitahidi kufanya mawasiliano na Mwigulu pasipo mafanikio, hata majuzi nilienda klabu ya Yanga kwa ajili ya ishu ya Deus Kaseke hawakugusia ishu ya Kenny.

"Walionyesha nia ya kuhitaji huduma ya Kenny ni KMC na ndio nimewapa kipaumbele, Singida United tunawadai mishahara ya Kenny ila kama wangekuwa na nia ya kumtaka Kenny isingezuia kuzungumza na Yanga.

"Nilivyoona kimya, niliandika barua kwenda Singida United kukumbusha juu ya kumalizika kwa mkataba wa mchezaji wangu pamoja na madai lakini walinijibu kuwa wanamtakia kila la kheri, ndiyo maana nilikubali mazungumzo na KMC," alisema Mwalwisi.