Kina Msuva gari limewaka

Monday May 18 2020

 

By ELIYA SOLOMON

BAADA ya miezi miwili kupita bila soka, Mtanzania Saimon Msuva ambaye anaichezea klabu ya Difaa El Jadida amesema wanatarajiwa kuanza mazoezi ya pamoja mwishoni mwa mwezi huu kujiandaa ili kuendelea na Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’ ambayo ilisimama kutokana na janga la virusi vya corona.

Msuva akiwa jijini El Jadida, alisema anasubiri siku ya kuripoti kambini maana ni kama dunia imeamua kuendelea na maisha huku corona ikichukuliwa sawa na magonjwa mengine ya kawaida lakini zitakuwa zikifuatwa tahadhari.

Mshambuliaji huyo mwenye mabao manne msimu huu katika Batola Pro, alisema kwa mujibu wa maelekezo waliyopokea kutoka kwa viongozi wao ni kwamba watafanyiwa vipimo mara mbili mbili kila mmoja wao.

“Viongozi wa soka la Morocco wamelenga tuendelee na Ligi huo ndio msimamo wao huku wakiangalia afya ya kila mchezaji. Haya ni maisha mapya ambayo tunapaswa kuendana nayo kwa sababu bado hakuna tiba rasmi ambayo wanasayansi wamepata pamoja na kazi kubwa walizofanya hadi sasa.

“Sijajua itakuwa lini lakini mwisho wa mwezi huu, Mei kutakuwa na mazoezi ya pamoja kama timu, tutaanza kufanya kwa makundi makundi lakini baada ya kufanyiwa vipimo,” alisema Msuva mwenye miaka 26.

Hata hivyo, Msuva ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga na Moro United za Tanzania, alisema ni wazi kuwa kila mmoja wao aliyakumbuka maisha ya kucheza soka kwa sababu haikuwa kawaida kukaa bila ya kucheza kwa muda mrefu kiasi hiki.

Advertisement

“Nilikumbuka kucheka na rafiki zangu kwa sababu vile ambavyo ninaishi na wachezaji wenzangu mzaha ni mwingi hata kama lugha ni gongana wengi huongea Kiarabu,” alisema.

Siku chache zilizopita Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco (FRMF) lilisema kwamba Ligi Kuu na mashindano ya nchi hiyo yataendelea tena katikati ya mwezi Juni.

Tofauti na nchi nyingine za Kiafrika ambazo ziliamua kuumaliza msimu wao wao mapema, Morocco imeamua kusubiri na kuanza tena kampeni yao mwezi Juni.

Shirikisho hilo likaongeza kuwa timu za daraja la juu kabisa nchini humo ambazo ni zile zinazoshiriki Ligi Kuu zitaruhusiwa kuanza mazoezi mwishoni mwa Mei kabla Batola Pro kurejea mwezi mmoja baadaye.

Ligi Kuu Morocco, ilisimamishwa katikati ya mwezi Machi baada ya raundi 20 kuchezwa kutokana na kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona vinavyoleta ugonjwa wa covid-19.

Advertisement