Kante akacha mazoezi Chelsea kisa corona

Friday May 22 2020

 

LONDON ENGLAND. KIUNGO wa Chelsea, N’Golo Kante ameruhusiwa kutofanya mazoezi na wenzake baada ya kuingiwa na hofu ya kuambukizwa virusi vya corona.

Kante alifanya mazoezi na wenzake Jumanne iliyopita, wakati Chelsea ilipokuwa moja ya timu zilizoanza mazoezi kujiandaa na mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Lakini, hakuonekana katika mazoezi ya Jumatano akiwa amepewa ruhusa na kocha Frank Lampard. Haifahamiki ni lini Mfaransa huyo atarejea kuungana na wenzake.

Uamuzi wa Kante umekuja baada ya kuripotiwa kwamba, kuna watu sita wamekutwa na maambukizi ya corona katika awamu ya kwanza ya Ligi Kuu England, kuwapima wachezaji pamoja na maofisa wa klabu kabla ya ligi hiyo kuanza upya.

Miongoni mwa hao waliokutwa na maambukizi, yupo kocha msaidizi wa Burnley, Ian Woan na beki wa Watford, Adrian Mariappa.

Mariappa ni moja kati ya watu watatu waliokutwa na maambukizi kwenye kikosi cha Watford huku mwenyewe akidai kwamba, hajui maambukizi hayo ameyapata wapi.

Advertisement

Mariappa alisema: “Tangu nilipopewa majibu Jumanne kwamba nimeambukiza virusi vya corona, nimebaki nakuna kichwa tu nikijaribu kufikiria ni wapo nilipata hii corona.

“Imekuwa sapraizi kubwa kwa sababu sikuwahi kutoka nyumbani, zaidi ya kufanya mazoezi tu na watoto.

“Daktari ameniita na kutaka nisema ukweli, nami niliuliza kama hii kitu ni sahihi kwa asilimia 100 au kama vipimo vyangu zimechanganywa. Pengine kama ningekuwa na dalili basi nisingekuwa na wasiwasi, lakini hapa nilipo sielewi virusi nimevipata wapi na kwa namna gani.

“Nikiwa na dalili zozote na mwenyewe nilijiona nipo fiti, tena fiti kuliko kawaida kwa sababu nilikuwa nafanya sana mazoezi. Nilikuwa naendelea tu na mazoezi na sikuwahi kupata tatizo la kupumua kuumwa au kitu kingine chochote kile. Lakini, nasikiliza wataalamu watanielekeza nini cha kufanya kwa sasa.”

Advertisement