Kagere? Tunahitaji kina Samatta wengii

MJADALA umekuwa ukiendelea nchini kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kuwa ama wawe watano au kumi katika kila timu. Wadau wametakiwa kutoa maoni yao, kuiwezesha mamlaka ya michezo nchini kuamua msimamo uwe upi.

Msingi wa mjadala wenyewe ni kuwa uamuzi utakaopatikana usaidie kuendeleza vijana wetu hapa nchini nao wawe wachezaji wazuri kwenye klabu zao na kwa timu ya taifa na hata kupata nafasi ya kucheza na kuajiriwa nje ya nchi. Madhumuni ni hatimaye Tanzania ipande chati katika mchezo wa soka duniani kuondokana na hali ya sasa ya kuwa duni katika eneo hilo tangu mpira wa ngazi ya klabu uanze nchini karibu karne moja iliyopita.

Kufikia sasa, sio klabu zetu wala timu ya taifa nchini, ukiacha Kombe la Mashariki mwa Afrika, hatujachukua Kombe la Afrika, wala la dunia. Wala Tanzania haijaingia katika kinyang’anyiro cha Kombe la Dunia ikilinganishwa na jirani zetu tunaopakana nao upande wa Kusini Magharibi na Magharibi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambao tayari wenzetu wameshayaonja mashindano ya Kombe la Dunia ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na wamekuwa wakila dola nyingi za shirikisho hilo.

Lakini, maswali ya msingi ya kujiuliza ni kuwa, kwanza, hivi ni kweli tutawaendeleza vijana wetu hapa nchini kwa kuruhusu katika ligi yetu kuwa na wachezaji wengi kutoka nje? Pili, je, siyo kweli kuwa vipaji vya vijana wetu vitanyanyuka kwa kuwaendeleza vijana kupitia shule maalum za kunoa vipaji hivyo na kuwapa misaada ya hali na mali wanayoihitaji?

Maoni yangu ni kuwa majibu ya hilo suala la pili hapo juu ndiyo ufumbuzi wa maendeleo ya soka nchini na siyo idadi ya wachezaji wa kigeni katika ligi nchini.

Katika miongo miwili mitatu iliyopita, timu zetu ziliwahi kusonga mbele vizuri, siyo kwa kuwa tulikuwa na wachezaji wa nje katika ligi, ila kulikuwa na maandalizi endelevu ya vijana wetu na wao wenyewe walijituma zaidi. Tusiwasahau makocha wazuri wa kigeni na mafunzo kama ya kanali mstaafu mwalimu Iddi Kipingu katika shule ya sekondari ya Jeshi, Makongo, jijiji Dar es Salaam. Wachezaji wawili wa Tanzania, Maulidi Dilunga na Omar Mahadhi, walitambuliwa na kujumuishwa katika timu ya soka ya Afrika, siyo kwa sababu ya kuwepo kwa wachezaji wa nje katika ligi yetu, ambao kamwe hakuwepo hata mmoja. Simba iliwahi kufika Fainali za Kombe la CAF kwa kukabiliana na Stella Artois ya Ivory Coast, siyo kutokana na wachezaji wa nje. Kina Kassim Manara, Sunday Manara, Kassim Matitu, Nico Njohole waliowahi kucheza soka hata nje ya nchi, hawakuhamasishwa na wachezaji wa kigeni katika ligi yetu. Hivi sasa, badala ya kuwaendeleza vijana wetu na kuwahamasisha wajitume, tunawaachia wakitumia muda mwingi zaidi katika saluni kujiremba na hasa kutengeneza nywele zao, badala ya kufanya mazoezi ya kujenga na kuimarisha miili yao. Sasa hivi, siyo kuwa wachezaji wa nje lazima wawe katika ligi yetu, tunawaona vizuri katika runinga na tunaweza tukaiga staili za uchezaji wao.

Wachezaji wa nje wako wengi katika ligi za Ulaya. Kwa mujibu wa habari mitandaoni karibu asiimia 60 ya wachezaji wote wa ligi za Ulaya ni wageni. Lakini sababu za wingi wao huko siyo kutaka kuhamasisha wachezaji wa ndani wa nchi hizo -Uingereza, Hispania, Ufaransa, Ujerumani, Italia Ubelgiji na Ureno bali ni kukuza biashara ya soka katika nchi hizo.

Na wachezaji wa kigeni wanakimbilia katika nchi hizo kwa sababu ya kupata fedha nzuri inayotokana na biashara kubwa ya mchezo huo inayofuatia uwekezaji mkubwa katika soka, matangazo ya televisheni na kamari kubwa ya mfumo wa kubeti!

Katika Mtandao wa Quora wa maswali na majibu, swali liliulizwa: kwa nini ni wachezaji wachache tu wa kigeni wanacheza katika ligi ya Brazil,moja ya nchi gwiji wa soka na iliyochukua Kombe la Dunia la Fifa mara tano, zaidi kuliko nchi nyingine yoyote.

Na jibu lililotolewa na mpenzi na mwandishi wa michezo, lilikuwa: Ligi ya Brazil ni ligi masikini kwa maana ya bajeti, mishahara midogo, mapato madogo ya matangazo katika televisheni, ikilinganishwa na ligi za nchi za Ulaya. Bajeti ya baadhi ya klabu kubwa za Brazil kama vile Corinthians, Flamingo na Sao Paulo, kwa mujibu wa Quora, ni ndogo zaidi mara 15 ikilinganishwa na bajeti ya baadhi ya klabu kubwa za Ulaya kama vile Real Madrid, Barcelona ama Manchester United.

Argentina, nchi nyingine gwiji wa soka duniani kutoka Bara la Amerika ya Kusini, kama ilivyo Brazil, hali inafanana. Ndiyo maana ligi ya Brazil haivutii wachezaji wa kigeni kama vile ligi za Ulaya.

Hata hivyo, Brazil ndiyo inayotoa wachezaji wengi kwa ligi za Ulaya kuliko nchi nyingine yoyote. Kwa mujibu wa Mtandao wa Statista, unaotoa takwimu za masuala ya michezo na burudani, hadi Novemba mwaka jana, kulikuwa na jumla ya wachezaji 466 wa Brazil katika ligi 31 za Ulaya. Wachezaji kama Ronaldo de Lima, Ronaldinho, Rivaldo Neymar walifanya vipaji vyao vijulikane na vikuzwe katika ligi za Ulaya. Aidha, takwimu zinaonyesha kuwa Brazil inasafirisha na kuuza wachezaji wengi zaidi duniani kuliko nchi yoyote duniani – wachezaji zaidi ya 600 kwa sasa.

Suala la wachezaji wa kigeni katika ligi mbalimbali duniani lina misimamo tofauti, kulingana na mahitaji ya eneo husika. Kwa mfano, ligi ya England ya English Premier League inayokuzwa na kutangazwa sana duniani, masharti ni kuwa katika wachezaji 18, lazima wawe miongoni mwao wachezaji sita “wa nyumbani”. Ligi ya Ufaransa, League 1, ina kiwango cha wachezaji wa kigeni watano tu katika timu na kwamba ni wanne tu wanaotakiwa wawe wanacheza uwanjani katika mechi moja yoyote. Ligi ya Ujerumani, Bundesliga, ilipoanzishwa mwaka 1963, ni wachezaji saba tu wa kigeni walioruhusiwa miongoni mwa wachezaji 300 wa ligi hiyo, lakini mpaka katika ligi ya mwaka 1915/16, miongoni mwa wachezaji wanataaluma 429, ni 194 tu Wajerumani wakati 235 wakiwa ni wa kigeni.

Ligi ya La Liga ya Hispania, kuna kanuni inayosema ni wachezaji watatu tu kutoka nje ya Umoja wa Ulaya, ndiyo wanaoruhusiwa kucheza katika ligi hiyo kwa timu.

Huko Brazil kwenyewe, wachezaji wa kigeni katika ligi yao naima jumla wako 22 tu. Tena wachezaji hao wa kigeni wengi ni kutoka nchi jirani na wamepata nafasi hiyo kuziba mapengo madogo madogo yaliyoachwa na nyota wa Brazil wanaosakata soka nje ya nchi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, kati ya hao 22, watano ni kutoka Argentina; Colombia (5); Chile (4); Uruguay (3); Paraguay (3) na mmoja mmoja kutoka Angola na Serbia. Tena ligi ya Brazil, kama ilivyo ya Argentina, ni ya mashindano makali ya vipaji kiasi kwamba wachezaji wa kigeni siyo rahisi kupata nafasi katika ligi hizo. Wachezaji wa Kiafrika, kwa mfano, pamoja na njaa yao kali kwamba wangeweza hata kukubali kulipwa ujira mdogo, wengi wao wasingepata namba na labda wangeishia kwenye mazoezi na kukaa benchi kama mashabiki tu.

Kwa hiyo, uchambuzi wa takwimu kuhusu wachezaji wa kigeni katika ligi za nchi mbalimbali hautoi picha yoyote kuwa wachezaji wa kigeni wanasaidia kunyanyua vipaji vya wachezaji wa ndani. Hakuna uhusiano kabisa kati ya kukua kwa vipaji vya wachezaji wa ndani na wingi wa wachezaji wa nje katika katika ligi za ndani.

Uingereza, kwa mfano, ligi yake ina wachezaji wengi wa nje lakini hao hawakuzi vipaji vya ndani, ila wanajipatia utajiri kutokana na biashara kubwa ya soka. Ndiyo maana timu ya taifa ya Uingereza, hata kuiunganisha kwake kuna kazi kubwa kwa vile hakuna wachezaji bora wa kutisha wa Kiingereza katika klabu za huko.

Ndiyo maana Uingereza, pamoja na ngebe yote kuhusu umaarufu wa ligi yake, imenyakua Kombe la Fifa la Dunia mara moja tu, tena kwa bahati, mwaka 1966, wakati mashindano hayo yalipofanyika kwao Uingereza.

Sana sana wanufaika wa ligi ya Uingereza ni wachezaji hao wa nje ambao wanapata pia uzoefu na kuzifanya timu zao za taifa wanakotoka kuwa tishio, hata kwa Uingereza yenyewe.

Ni kweli Ujerumani nayo ina wachezaji wengi wa kigeni katika ligi yake na ina timu bora ya taifa. Lakini ubora wa timu ya taifa ya Ujerumani hautokani na kukolezwa na wageni, bali ni mfumo wa Ujerumani yenyewe wa kukuza vipaji vya vijana wake katika timu za wale walio chini ya miaka 15, 17, 20 na 21.

Fifa, inafahamika, inatoa dola nyingi kila mwaka kwa mashirikisho ya soka ya kitaifa, likiwamo la Tanzania, kuendeleza soka la vijana. Lakini fedha hizo mara nyingi haizielezwi zimekuja ngapi, lini, zimetumikaje.

Inafahamika pia wakati fulani Fifa ilisimamisha mgao kwa Tanzania kutokana na wanaopewa fedha hizo kushindwa kueleza vizuri matumizi yake.

Kwa hiyo ni dhahiri kuwa misaada kama hiyo ya Fifa, kuanzisha shule nyingi za kuendeleza vipaji vya soka, kuwa na utawala mzuri na wa kisasa katika klabu za soka na shirikisho ndiko kutakakoipaisha Tanzania katika soka na siyo kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni katika ligi.

Watakaonufaika na kuongezeka kwa idadi ya wachezaji wa kigeni hapa nchini ni wale wanaowaleta wachezaji hao na kuisimamia mikataba yao. Tukiendeleza soka nchini na sisi vijana wetu watapata nafasi zaidi kwenda kucheza nje. Tutakuwa na kina Mbwana Ali Samata wengi zaidi na ndiyo itakuwa faida kwetu, na siyo kuwa na kina Meddie Kagere na Morrison wengi zaidi, wanaoendelea kututia hasara kwa kuwalipa fedha nyingi zaidi kuliko zile tunazozitumia kuwaendeleza vijana wetu.

Labda kama tunataka ligi yetu iwe kama ya Uingereza, jambo ambalo haliwezekani, kwa kuwa hatuna miundombinu ya kutuwezesha kufikia huko.

Mwandishi ni mwanahabari mkongwe nchini na aliwahi kuwa Mhariri wa

Magazeti ya UHURU na MWANANCHI. Anapatikana kwa Barua-pepe: [email protected] na Simu: 0754-388418.