Kagere, Okwi freshi ila kazi wanayo TU!

Friday May 10 2019

 

By THOBIAS SEBASTIAN NA OLIPA ASSA

KAMA unadhani habari ya mjini ni ushindi wa mabao 8-1 iliyopata Simba dhidi ya Coastal Union katika Ligi Kuu Bara umekosea. Pia kama unadhani ni zile comeback walizofanya Liverpool kwa Barcelona ama ile ya Spurs dhidi ya Ajax Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia jua umechemsha.

Gumzo la sasa ni hat trick mbili kwa mpigo zilizopatikana kwenye pambano la Simba na Coastal, huku zote zikipigwa na nyota wa kigeni wa klabu hiyo, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi. Ni muda mrefu katika ligi hiyo haijashuhudiwa wachezaji wawili kufunga hat trick katika mechi moja, lakini utamu zaidi ni mabao matatu ya kila mmoja ya nyota hao wa Simba yamewafanya kuweka rekodi binafsi kwa wachezaji hao.

Kagere akiifikia rekodi ya Okwi ya msimu uliopita alipotwaa tuzo ya Mfungaji Bora kwa idadi ya mabao 20 ambayo ameyafikisha baada ya kufunga hat trick yake hiyo juzi Uwanja wa Uhuru. Pia mabao matatu Okwi yamemfanya kuandikisha rekodi mpya kwake ya kufunga hat trick mbili katika msimu mmoja Ligi Kuu Bara kwani kabla ya hapo alikuwa hajawahi kufanya hivyo licha ya kucheza nchini tangu mwaka 2010.

Hat trick ya juzi ilikuwa ya tatu kwa Okwi kwani msimu uliopita alifunga moja dhidi ya Ruvu Shooting na msimu huu kapiga mbili dhidi ya Ruvu na dhidi ya Coastal na kusaliwa na tatu tu amfikie Amissi Tambwe wa Yanga aliyefunga hat trick sita.

KAZI IPO HAPA

Lakini unaambiwa, kasi ya nyota hao wawili sio tu imewashtua nyota wanaochuana nao kwenye mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu cha msimu huu, pia hata nyota wa zamani wameshtushwa kwani, ni kama majamaa wanaenda kuvunja rekodi iliyodumu kwa muda mrefu katika historia ya Ligi Kuu.

Advertisement

Ndio kama hujui, huu ni mwaka wa 20, tangu rekodi ya mabao 26 katika msimu mmoja, iliyowekwa na straika wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ bado haijavunjwa na mastaa wazawa na wa kigeni waliocheza ligi hiyo.

Mmachinga aliiweka mwaka 1998 na mkali mwingine wa mabao aliyewahi kutamba nchini, Abdallah Juma aliyekuwa akikipiga Mtibwa Sugar alikaribia kuifikia kwa kufunga mabao 25 katika msimu wa 2005 na baada ya hapo hakuna aliyewahi kuisogelea.

Kwa kasi ya Kagere, huku akiwa na mechi nyingi mkononi kabla ya msimu kumalizika ni kama vile straika huyo anaenda kuweka rekodi mpya ambayo huenda ikachukua muda mrefu nayo kujka kuvunjwa.

Kagere ana mabao 20 kwa sasa na mechi saba mkononi na kama atatupia kama anavyofanya kwa sasa huenda akaivuka ile ya Mmachinga, jambo ambalo nyota huyo wa zamani aliyewahi pia kukipiga Simba, Bandari Mtwara na Taifa Stars alifunguka.

MSIKIE MWENYEWE

“Meddie, Bocco na Okwi ni washambuliaji wazuri ili waweze kuvunja rekodi yangu wanatakiwa kuwa na wivu wa kutamani kuivunja kwani imedumu kwa miaka mingi, jambo ambalo naliona msimu huu wameamua kufanya hivyo na kwa mechi zilizobaki wanaweza kuifikia au kuivunja kabisa kama wasipopata matatizo yoyote katika mchezo yao saba waliyobaki nayo,” alisema.

“Wakati nacheza na nikaweza kufunga mabao 26, soka lilikuwa halilipi kama wakati huu lakini nilijituma kutimiza malengo ya timu kufanya vizuri ambayo yalikuwa yanafanikiwa na baada ya hapo nafasi za kufunga zilikuwa zinakuja ndio tu ndio nikaweza kufikisha idadi hiyo ya mabao.

“Rekodi hiyo inaonyesha heshima ya wachezaji wa zamani namna ambavyo tulikuwa tunajituma kuonyeshana uwezo uwanjani, tuliuheshimu mpira na ukatuheshimu kwani watu walikuwa wanapata burudani ya maana,” alisema Mmachinga.

TAMBWE HANA CHAKE

Kama hujui tu, nyota wa kigeni aliyekuwa akishikilia rekodi ya kufunga mabao mengi na kumkaribia Mmachinga na Juma ni straika wa Yanga, Amissi Tambwe msimu wa 2015-16, aliyomaliza akiwa Mfungaji Bora na mabao 21.

Tambwe aliweka rekodi hiyo baada ya nyota wengi wazawa na wa nje walikuwa wakiishia kufunga mabao kati ya 17-19 na Okwi akajitutumua msimu uliopita kwa kufunga 20. Hata hivyo ana kitu kimoja cha kujivunia, kama rekodi ya mabao 21 kwa nyota wa kigeni ikivunjwa na Kagere na Okwi, bado watakuwa na kazi ya kuifukuzia rekodi yake tamu ya kupiga ha trick sita katika misimu yake sita ya kucheza Ligi Kuu Bara.

AJ HUYU HAPA

Abdallah Juma ‘AJ” anafunguka kwa kudai wachezaji wa kizazi cha sasa wanashindwa kujitambua na hasa wazawa akidai hakuna kitu kibaya kama washambuliaji wa kigeni kufunga wao mara kwa mara na kutwaa tuzo ya ufungaji bora huku wazawa wakiwa wanaendelea kulizika na kulishuhudia hilo.

“Ninachowashauri washambuliaji wazawa wanatakiwa kuwa na juhudi binafsi na timu, pia wawe na wivu wa maendeleo kutamani kufanya kama ambavyo tulifanya sisi wakati tunacheza na si kuacha washambuliaji wa kigeni wakifanya vizuri wao msimu mingi.”

KAGERE, OKWI WAFUNGUKA

Kuhusu ishu ya kufunga na kutaka kuvunja rekodi, Kagere anafunguka kwa kudai, alisajiliwa timu yake lengo la kwanza ilikuwa ni kuutetea ubingwa huo, ila kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufika katika hatua ya makundi ambayo waliifanikisha.

“Uwezekano wa kufunga mabao zaidi ya mfungaji bora wa msimu uliopita upo kwani bado mechi ni nyingi lakini inaweza nisifanye hivyo nikashirikiana na wenzangu Okwi na Bocco ambao nao wanauwezo wa kufunga zaidi ya msimu uliopita,” alisema Kagere.

“Safu ya ushambuliaji wa Simba msimu huu imekuwa ikifanya kazi yao vizuri si mimi peke yangu na nina matumaini mmoja wetu ndio anaweza kutwaa tuzo ya mfungaji bora.”

Naye Okwi alisema anajisikia faraja kupiga hat trick yake ya tatu akidai imetokana na hali ya timu kuwa kwenye kiwango cha juu na kucheza kwa ushirikiano ambao tumekuwa tukishirikiana na wachezaji wanzangu katika kila mechi.

“Kikubwa ni ushirikiano wa kuifikisha Simba kwenye malengo muhimu ya msimu huu, kuhusu hat-trick ni mambo yanayozaliwa tukiwa kwenye mapambano ya kutimiza majukumu ya timu,” alisema Okwi.

Advertisement